Msanii maarufu ambaye pia ni mwanasiasa, Robert kyagulany anayejulikana kama Bob Wine ameongoza maandamano ya kupinga kodi iliyoanza kutozwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Uganda.

Kwa mujibu wa kodi hiyo mtumiaji anatakiwa kulipa shilingi 200 za Uganda kila siku kutumia facebook, Whatsapp, Instagram, Twitter na kadhalika.

Wanaharakati pamoja na waandishi wa habari wameshiriki maandamano hayo ambayo yalikuwa ya amani.

Polisi wametawanya maandamano hayo kwa kufyatua gesi ya kutoa machozi na risasi hewani kutawanya waandamanaji hao wanaopinga kodi hiyo.

Hata hivyo Polisi walijaribu kumkamata mbunge, Robert Kyagulany maarufu kama Bob Wine bila mafanikio kwani mbunge huyo alikimbilia bungeni ambapo polisi hao walishindwa kumkamata.

Aidha kodi hiyo ya mtandaoni iliidhinishwa mwanzoni mwa mwezi huu Julai 1, 2018 ikiwa na lengo la kuwataka watumiaji kulipia gharama hizo ili waweze kutumia mitandao hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika mara baada ya kuanza kutekeleza sheria hiyo, watumiaji wa mitandao ya kijamii wameonekana kupungua kwa takribani asilimia 75, ambapo wafanyabiashara wadogo wamelalamika kuathiriwa na sheria hiyo.

Rais Museveni amesema kwamba kodi kwa mitandao ya kijamii inaweza kuongeza kipato cha serikali, na kupunguza mikopo inayochukua serikali na pesa za ufadhili.

Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine
Cardi B na Offset wamkaribisha duniani mtoto wa kike