Mbunge wa Kilwa Kusini, kupitia chama cha Wananchi (CUF), Suleiman Bungara maarufu kama ‘Bwege’, amesema kuwa alishikiliwa na Polisi kwa muda kufuatia kutoa kauli ambayo imeonekana kupishana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, kuhusiana na suala la vitambulisho vya mjasiriamali mdogo.

Bwege amesema kuwa kilichomponza ni hatua yake ya kuwataka wavuvi wasinunue vitambulisho, kwa kile alichokidai kuwa inatokana na wao kutokuwepo kwenye kundi la wajasiriamali wadogo wadogo.

“Ni kweli nilikamatwa tatizo ni suala la vitambulisho vya ujasiriamali mimi na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, hoja yangu ilikuwa wavuvi si wajasiriamali kwa sababu yeye anakata leseni ya uvuvi na haruhusiwi kwenda baharini, lakini mjasiriamali ni mfanyabiashara mdogomdogo lakini RC aliwataka wavuvi wanunue vitambulisho mimi niliwaambia walipe 23,000 tu ya leseni.” amesema Mbunge Bwege.

Aidha, amesema kuwa alishangaa kupigiwa simu na OCD wa Kilwa kuwa amepingana na kauli ya RC kuwa ametoa kauli ya kichochezi na walimchukua na kumuweka ndani  lakini baadaye alitoka kwa dhamana.

Disemba 10, 2018 Rais Magufuli alingilia kati sakata la kutotambuliwa kwa wafanyabiashara wadogo nchini kwa kuchapisha vitambulisho maalum kwaajili ya kuwatambua wafanyabiashara hao ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru na kuvikabidhi kwa wakuu wa mikoa.

Tuhuma 13 za Mkurugenzi Ileje kuchunguzwa
Video: Kitine amchambua Membe Urais CCM, Rais mstaafu aenda upinzani