Mbunge wa viti Maalumu Chadema, Upendo Peneza amewaomba wananchi waliombee Taifa liendelee kuwa na amani pamoja na kuwaombea viongozi wa kisiasa wawe na uvumilivu  ili wazidi kusonga mbele kimaendeleo.

Peneza amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Likangara wilayani Ruangwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mkoani Lindi.

“Wananchi wa Ruangwa nawatakia maisha mema ili mzidi kusonga mbele,  tuombee amani ya nchi yetu na mtuombee viongozi tuwe na uvumilivu wa kisiasa.”

Pia katika mkutano huo walikuwepo wabunge wengine ambao ni, Hassan Masala (Nachingwea), Zubery Kuchauka (Liwale), Hassan Kaunje (Lindi Mjini) na Hamida Abdalaah (Viti Maalumu) ambao wote kwa pamoja wamesema lengo la kushiriki kwenye ziara hiyo ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliwataka wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanaendelea kudumisha na kuilinda amani iliyoko kwa sababu ndiyo inayowawezesha kufanya shughuli zao za kimaendeleo.

Amesema licha ya kuwepo kwa matukio machache ya uhalifu yanayojitokeza katika baadhi ya maeneo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na mikoa jirani limejizatiti kukabiliana na wahalifu wa aina yoyote kwa mtu mmoja mmoja au vikundi.

Mbowe: Upinzani ni wito
Walimu wakuu mbaroni kwa kufanya vikao na Al-Shabaab