Mbunge wa Jimbo la Longido kwa tiketi ya Chadema, Onesmo Ole Nangole amekana elimu ya sekondari inayomtambulisha kwenye tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania.

Mbunge huyo alikana elimu hiyo Katika Mahakama  Kuu jijini Arusha katika kesi ya kupinga matokeo ya jimbo hilo wakati akijibu maswali ya Wakili Dk. Masumbuko Lamwai.

Dk. Lamwai alimuuliza Mbunge huyo kiwango chake cha elimu akirejea elimu ya Sekondari iliyoandikwa kwenye wasifu wake katika Tovuti ya Bunge.

Alisema kuwa anafahamu tovuti hiyo imeonesha kuwa amesoma Sekondari ya Arusha, lakini ukweli ni kwamba yeye hajawahi kusoma sekondari bali alimaliza elimu ya msingi na kujiendeleza baadae katika chuo cha Lushoto kuhusu masuala ya Siasa.

Mbali na hilo, Mbunge huyo pia alikana mwaka wa kuzaliwa ulioandikwa katika tovuti ya Bunge inayoonesha kuwa amezaliwa mwaka 1958 akieleza kuwa ukweli ni kwamba yeye alizaliwa mwaka 1956.

Naye Wakili wa upande wa mlalamikiwa, Method Kimomogolo alimuuliza mbunge huyo kuhusu taarifa hizo zinazokanganya akitaka kujua nani aliyezipeleka Bungeni.

“Nani anatuma taarifa zako za Bunge?” Aliuliza Kimomogolo. “Mimi,” alijibu Ole Nangole. “Nani anajaza kwenye tovuti ya Bunge?” aliuliza tena. “Katibu wa Huduma za Bunge,” alijibu tena Ole Nangole.

Ole Nangole alikuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Monduli tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2005, lakini mwaka jana alihamia Chadema akimfuata waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Aligombea ubunge wa jimbo la Longido kwa tiketi ya Chadema na kumshinda Dk. Steven Kiruswa (CCM).

Video: Obama amuidhinisha Hillary Clinton Urais wa Marekani
Video: Serikali imepata gawio la bilioni 23 la ubia kutoka Puma, NMB na Tiper