Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete kwa kushirikiana na halmashauri ya Chalinze, wametoa magodoro 200  yaliyogharimu zaidi ya mil.8 ili kuwasaidia wanafunzi wa shule ya sekondari ya Moreto iliyopo Lugoba wilayani Bagamoyo.
Aidha Ridhiwani ameahidi kushirikiana na wadau pamoja na halmashauri hiyo, kujenga bweni jipya la wanafunzi wa kike, shuleni hapo baada ya kuunguliwa na bweni wiki iliyopita.
Sambamba na hayo tathmini imebaini hasara ya shil.mil. 74 baada ya bweni hilo kuungua  na kusababisha mali zote kuteketea kwa moto.
Akikabidhi magodoro hayo , kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Justine Lyamuya , mbunge huyo alisema kati ya magodoro hayo 136 yatatumiwa na wanafunzi wa kike na yatakayobaki yatatumika na wanafunzi wa kiume.
Ridhiwani alisema mara baada ya kutokea kwa janga hilo, alitoa magodoro 50 yenye thamani ya mil.2.2 kwa nguvu zake mwenyewe.
Hata hivyo aliwataka wanafunzi hao kushirikiana na serikali na vyombo vya dola kuwafichua waliohusika na tukio la kuchoma moto bweni.
Ridhiwani alielezea kuwa serikali itahakikisha waliohusika kuchoma moto bweni hilo,wanatafutwa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Alisema tukio hilo linasikitisha na kurudisha nyuma juhudi za serikali na wadau mbalimbali wa elimu wanaohakikisha  wanafunzi wanakaa bweni .
“Tumeweka mikakati ya kuhakikisha tunawakamata wale wote waliohusika na tukio hili baya na matukio haya ni mwendelezo wa uunguzaji wa shule ambapo Chalinze imechomwa mara mbili,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kushirikiana kutatua changamoto zilizojitokeza shuleni humo.
Nae  mwalimu mkuu wa shule hiyo Justine Lyamuya alifafanua kuwa vitu vyote viliungua ikiwa ni pamoja na vitanda na magodoro 75 vyenye thamani ya mil. 24.
Alisema bweni hilo lilijengwa hivi karibuni kwa thamani ya mil.50 ambalo limeungua lote na halifai tena kutumika.
“Moto huo uliunguza vitu vyote vilivyokuwemo ikiwepo magodoro, vitanda 75, madaftari, vitabu, nguo na vifaa vingine lakini mungu alisaidia kati ya wanafunzi 196 wanaolala bweni hili,hawakuwepo bwenini,” alisema Lyamuya.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze,Said Zikatimu alisema licha ya kuchangia magodoro hayo tayari wameitisha kikao na wazazi, walezi na wadau wa elimu ili kujadili namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
Baadhi ya wanafunzi Sekion Mponela na Mwanahamis Msonde walimshukuru mbunge wa Chalinze na halmashauri kwa msaada walioutoa na kuahidi kutunza magodoro hayo.
Octoba 5 mwaka huu majira ya asubuhi moto ulizuka katika bweni la wanafunzi wa kike shuleni humo na kusababisha hasara kubwa.

Madereva wa Magari Yabebayo Mchanga Mkoa wa pwani Wailalamikia Tanroads
Video: 'Rais Magufuli ni mtanzania wa pekee sana' - DC Hapi