Mbunge wa jimbo la Starehe, Charles Njagua maarufu kama Jaguar amekamatwa leo nje ya jengo la Bunge la Kenya, kutokana na kauli yake aliyoitoa akiwataka Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda kuondoka nchini humo ndani ya saa 24 vinginevyo watapigwa.

Kwa mujibu wa Citizen TV, Njagua amekamatwa majira ya saa sita na nusu kwa saa za Afrika Mashariki na askari polisi waliokuwa wamevaa kiraia na kisha kupandishwa kwenye gari la polisi.

“Kama utatembelea masoko, Waganda na Watanzania dio waliochukua biashara yote. Sasa tunasema imetosha. Kama wataona muda wa saa 24 wa kuondoka haraka nchini hautoshi, tutawaondoa kwa nguvu na tutawapiga na hatutamuogopa mtu,” alisema Njagua alipotembelea masoko.

Kauli hiyo ilisababisha taharuki ya kidiplomasia kati ya nchi za Afrika Mashariki.

Jana, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliliambia Bunge kuwa Serikali imezungumza na Balozi wa Kenya nchini pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya kuhusu kauli hiyo. Alisema kuwa Serikali ya Kenya imeeleza kuwa kauli ya Njagua sio  msimamo wa Serikali na kwamba ni kauli yake binafsi.

Hata hivyo, jana Njagua aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter akieleza kuwa hakumaanisha Watanzania na Waganda, jambo ambalo lilisababisha watu wengi wamshambulie.

“Kauli zangu zilikuwa zinaunga mkono maelekezo ya Waziri Matiang’i yakimaanisha Wachina waliongia kwenye masoko yetu kufanya biashara, hali ambayo haivumiliki kwa wananchi. Siko kinyume na muungano wa jumuiya [ya Afrika Mashariki] unaohuisha biashara kati ya jumuiya hiyo,” alitweet.

Juni 12, 2019, Waziri Matiang’i aliagiza kuondolewa mara moja kwenye masoko wafanyabiahara wa kigeni [hasa Bara Asia] ambao wanafanya biashara za kawaida kwenye masoko ya Kenya.

Hatua hiyo ya Matiang’i ilikuwa ikijibu kilio cha wafanyabiashara wa Kenya ambao walidai kuwa Wachina wameingia kwenye soko la Nairobi la Gikomba kufanya biashara kinyume cha taratibu ambazo zinawataka kuwa wawekezaji kwa kiwango fulani cha mitaji.

Benki ya Wakulima TADB kukifufua kiwanda cha TANICA mkoani Kagera
Fahamu sababu ya maumivu kwenye korodani kuwa chanzo cha ugumba

Comments

comments