Mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya Chadema, Jessica Kishoa ametolewa nje ya Bunge na kuamriwa kutohudhuria vikao viwili vilivyobaki kwa kosa la kulidanganya Bunge.

Kabla ya kuchukua uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alilieleza bunge hilo kuwa mbunge huyo alishindwa kuwasilisha ushahidi wa madai yake aliyoyatoa bungeni humo Februari 1 kuhusu gharama za manunuzi ya mabehewa 274 aliyodai yalikuwa mabovu.

Kishoa alisema kuwa mabehewa hayo yaligharimu shilingi bilioni 238, gharama ambazo zilipingwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe ambaye wakati wa manunuzi alikuwa waziri wa uchukuzi. Mwakyembe alidai kuwa gharama za manunuzi hazikuzidi bilioni 60. Kishoa alipewa siku tatu kuwasilisha ushahidi wake.

Leo, Mwenyekiti wa Bunge alimtaka Kishoa kufuta kauli yake baada ya kushindwa kuwasilisha ushahidi lakini Mbunge huyo alikataa akimtaka Mwakyembe kuthibitisha gharama alizozitaja kwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

“Mheshimiwa, kwakuwa kanuni hii inanitaka kumsimamisha mheshimiwa mbunge kwa siku zisizozidi 5. Na kwakuwa tumebakiwa na siku mbili tu kabla ya kumaliza mkutano wa pili wa bunge, namsimamisha mheshimiwa Jesca Kishoa kutohudhuria vikao viwili vya bunge vilivyosalia, kuanzia sasa hivi,” alisema Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge.

 

Akiwa nje ya bunge muda mfupi baada ya kutolewa na mwenyekiti huyo, Kisho alieleza sababu za kukataa kufuta kauli yake.

“Nimekataa kufuta kauli kwa sababu, kama kweli haya mambo hayana ushahidi. Kulikuwa na njia moja tu ambayo ni kuleta ripoti Bungeni. Ile ripoti ya PPRA inasema hivi, ununuzi wa mabehewa haukufuata utaratibu,” alisema Kisho huku akisisitiza kuwa hata acha kufuatilia suala hilo hata kama angetolewa bungeni kwa siku 10.

Alisema kuwa aliomba apatiwe ripoti ya PPRA kuhusu ununuzi wa mabehewa hayo lakini hakupewa ushirikiano na ofisi za bunge.

Lowassa atoa ombi lake kwa Rais Magufuli, Bado anauona mlango wa ikulu
Lukuvi awamwagia sifa Zitto na Mbatia, awaponda wengine kwa hili