Bingwa wa mapigano ya mchanganyiko wa masumbwi na mieleka, Conor McGregor ambaye leo alipigwa na Floyd Mayweather katika raundi ya 10 amemlalamikia muamuzi wa pambano hilo kwa kumaliza pambano.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa pambano hilo, McGregor amedai kuwa muamuzi angemuacha aendelee kwani alikuwa na uwezo wa kumaliza raundi zote 12 lakini alikuwa amechoka tu.

“Kulikuwa na mengi bado kwenye mstari na nilitakiwa niachwe niendelee. Mwanzoni kabisa nilikuwa nimefanya mengi ya kutosha. Lilikuwa pambano la ushindani wa karibu,” alisema McGregor.

“Jamaa (muamuzi) angeniacha niendelea, angemuacha jamaa (Mayweather) aniangushe chini. Ulipaswa kuniweka chini. Nafurahi kupambana katika aina nyingine ya mashabiki na kuwa hapa nikipeperusha bendera,” aliongeza.

Kwa upande wa Mayweather ambaye ametangaza kustaafu tena na kutorudi tena kwenye masumbwi alimpongeza McGregor akieleza kuwa alikuwa mshindani hodari na shupavu.

“Alikuwa mpambanaji shupavu na nadhani tumewapa mashabiki walichokuwa wanataka kukiona. Alikuwa na uwezo mkubwa zaidi ya nilivyodhani, alikuwa anatumia kona mbalimbali. Alikuwa mshindani shupavu na mgumu lakini nilikuwa bora zaidi usiku wa leo,” aliongeza.

Mayweather amesema kuwa siri ya ushindi huo ni kumpa nafasi za raundi ya kwanza McGregor kurusha masumbwi yake yote ambayo huyarusha katika mapigano ya MMA ambayo huchukua dakika 25 tu na kwamba baada ya hapo angemmaliza.

Matokeo ya majaji yameonesha kuwa hadi raundi ya 10, Mayweather alikuwa ameshinda raundi 8 kati na McGregor 4.

Nchemba awaweka mtegoni bodaboda, abiria
‘Seduce Me’ ya Ali Kiba yavunja rekodi Afrika Mashariki