Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema kuwa utaratibu wa kupata cheti mbadala/uthibitisho kwa mtu aliyepoteza cheti utakuwa ukifanyika ndani ya siku 30.

Ameyasema hayo hii leo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) lililokuwa likihoji ni utaratibu gani unaotumika pale mtu anapopoteza cheti ili aweze kupata cheti kingine.

Amesema kuwa mhitimu aliyepoteza cheti hupatiwa cheti mbadala/uthibitisho wa matokeo kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu.

Aidha , amesema kuwa mtu aliyepotelewa na cheti atatakiwa kutangaza gazetini kuhusu upotevu huo  kwa lengo la kuutaarifu umma ili kusaidia kukipata na endapo cheti hakitapatikana hata baada ya kufuata utaratibu huo ,mhitimu atajaza fomu ya ombi la cheti mbadala /uthibitisho wa matokeo na kuiwakilisha Baraza la Mitihani.

‘’Baada ya mhitimu kujaza fomu hiyo Baraza la Mitihani hufanya uchunguzi wa uhalali wa umiliki wa cheti husika na kutoa huduma stahiki, wahitimu waliofanya mtihani kuanzia Mwaka 2008 ambao vyeti vyao vina picha hupatiwa vyeti mbadala,‘’amesema Ole Nasha

Hata hivyo, cheti mbadala kinachotolewa ni cheti halisi ambacho huongezwa maandishi yanayosomeka ’DUBLICATE’ kuonyesha kuwa cheti hicho kimetolewa mara ya pili.

Nembo ya umoja wa wanamitindo yazinduliwa
Nyumba ya kiongozi wa NASA yashambuliwa Kenya