Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uingereza, Jermaine Jenas ameponda uamuzi wa Klabu ya Manchester United kumpa ajira ya kudumu Meneja Ole Gunnar Solskjaer.

Jenas ambaye aliwahi kuchezea klabu za Newcastle United, Tottenham Hotspur, Aston Villa na Queens Park Rangers amesema kuwa anadhani klabu hiyo haikujua inachofanya wakati wa kufikia uamuzi huo ambao amedai ulitokana na kuzidiwa hisia kwa mafanikio ya awali ya Solskjaer.

Solskjaer aliibeba Manchester United katika kipindi cha mpito akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Jose Mourinho ambaye alifukuzwa Desemba mwaka jana baada ya kupata matokeo mabaya mfululizo.

Kocha huyo mwenye rekodi ya kushinda Kombe la Mabingwa akiichezea klabu hiyo mwaka 1999 aliingia na bahati ya aina yake akishinda michezo 10 kati ya 11, hatua iliyowavutia Manchester United na kumtunuku mkataba wa kudumu Machi mwaka huu.

Lakini hivi karibuni bundi ametua kwenye kazi ya meneja huyo, ambapo ameshapoteza michezo mitano kati ya michezo saba ikiwa ni pamoja na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona. Hali hiyo ndiyo iliyomfanya Jenas kukosoa uamuzi wa Wekundu hao wa Old Trafford.

“Mimi nadhani ulikuwa uamuzi wa kihisia zaidi, lakini kwenye biashara kunapaswa kuwa na uamuzi unaofikiria muda mrefu ujao. Alichokifanya Alex Ferguson kilikuwa cha kipekee sana na United wamekuwa na wakati mgumu sana kumpata meneja kama yeye,” Janes amewaambia waandishi wa habari.

“Pep Guardiola alipoenda Manchester City hakusema ‘Roberto Mancini na Manuel Pellegrini walifanya nini kushinda Ligi? Aliingia na kufanya kile ambacho alitaka kufanya. Lakini nadhani Manchester United hawajui wanachokifanya sasa,” aliongeza.

Klabu hiyo hivi sasa iko katika nafasi ya sita kwenye Ligi ikiwa na alama mbili nyuma ya Arsenal na Chelsea ambao wako katika nafasi ya nne na tano.

Kinachofuata kwa Mashetani Wekundu ni mtanange mwingine dhidi ya Everton Jumapili hii wakiwa ugenini.

Leo ni leo: Amir Khan kuzichapa na Terrence Crawford
Video: Tazama maana ya neno "MISSED CALL" 😂 / Walivyotamka neno "CHARACTERISTIC" 😂🤣

Comments

comments