Shirikisho la soka duniani FIFA, limemfungia maisha mchezaji wa Uganda George Mandela, baada ya kubainika alihusika kwenye harakati za upangaji wa matokeo, wakati alipokua akiitumikia klabu ya Kenya Kakamega Home Boyz.

FIFA wamejiridhisha kuhusu tuhuma zilizokua zikimkabili mchezaji huyo mwaka jana (2019) na imebaini kupitia ushahidi waliopata, huku wakiamini adhabu hiyo itakua fundisho kwa wachezaji na wadau wenye dhamira ya kupanga matokeo.

Pia FIFA imetangaza kuwafungia miaka minne wachezaji wengine watatu kutoka Kenya Moses Chikati, Festus Okiring na Festo Omukoto, kufuatia kuhusika kwenye sakata hilo la upangaji wa matokeo.

“FIFA imejiridhisha na kubaini ukweli wa harakati za upangaji wa matokeo, na imemkuta na hatia mchezaji Mandela, ambaye alikua kinara kweye mpango wa kwenda kinyume na taratibu za mchezo wa soka, kwenye baadhi ya michezo ya ligi ya Kenya mwaka 2019,” imeeleza taarifa iliyotolewa na FIFA.

“Uchunguzi uliofanywa umebaini mambo mengi na hadi maamuzi ya adhabu hizo yanatangazwa, tunaamini itakua fundisho kwa wachezaji wengine na wadau wa soka duniani wenye dhamira ya kupanga matokeo.”

FIFA imekua mstari wa mbele kupinga vitendo vya upangaji wa matokeo kwa madai ya kutaka kuona usafi unasalia kwenye mchezo huo pendwa duniani.

Tayari maelfu ya wadau wa soka duniani wameshakumbana na adhabu, baada ya kubainika walihusika kwenye kashfa ya upangaji matokeo.

Video: HARMONIZE anaweza kuishiwa muda si mrefu? |Video mpya ya MARIOO YAIBUA ajabu lingine
TFF yakanusha kufuta sheria namba 11 ya soka