Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 40 walijeruhiwa kabla ya mchezo wakuwania nafasi ya kushiriki fainali za Afrika (AFCON 2019) kati ya Madagascar dhidi ya Senegal uliounguruma jana mjini Antananarivo.

Taarifa kutoka hospitali ya manispaa ya De Mahamasina mjini Antananarivo zimeeleza kuwa, waliojeruhiwa wameumizwa vibaya. Ripoti waliyoipata imeeleza kuwa hatua hiyo ilisababishwa na fujo zilizotokea wakati wakijaribu kuingia uwanjani.

Mamlaka ya soka nchini Madagascar imetoa taarifa za kuthibitisha kutokea kwa fujo hizo, ambazo zilitokana na idadi kubwa ya mashabiki kuhitaji kuingia uwanjani wakati tayari idadi ya mashabiki waliokua ndani ilikua imeshatosha.

Uwanja wa taifa nchini humo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 22,000 ulifurika kabla ya mchezo dhidi ya Sengal, na wengine wanaokadiriwa kufikia 1000 bado walikua nje na walilazimisha kuingia ndani.

“Mashabiki walilazimisha kuingia ndani, watu wa usalama walijitahidi kuwazuia na kufanikiwa, lakini kusukumana na kukanyagana kulisababisha kupatikana kwa majeruhi kadhaa na mmoja alifariki dunia,” alieleza mkuu wa jeshi la polisi Herilalatiana Andrianarisaona, alipohojiwa na kituo cha Radio cha Ufaransa cha RFI.

“Kulikua hakuna ustahamilivu baina ya mashabiki waliokua nje ya uwanja, tuliwasihi kurejea nyumbani na kuufuatilia mchezo huo kupitia televisheni lakini zoezi hilo walilikaidi na kuendelea kusukumana.”

Tayari waziri wa michezo nchini Madagascan Tsihoara Faratiana, waziri wa ulinzi na viongozi wa shirikisho la soka wamefika hospitalini kuwatembelea na kuwajulia hali majeruhi wa tukio hilo.

Mchezo kati ya Madagascar dhihi ya Senegal ilimalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Video: Benki kuu yajibu hoja ya Zitto, Magufuli amgomea Waziri wake
Hapi agoma kuzindua Jengo