Mfanyabiashara mmoja raia wa China amekumbwa na adhabu ya kulipa faini kwa kosa la kuuza bendera za taifa la Zimbabwe, kinyume cha maagizo ya Serikali.

Kwa mujibu wa gazeti la Herald, mfanyabiashara huyo aliyetajwa kwa jina la Weidong Li alitiwa mbaroni pamoja na bendera 314 za taifa hilo na mahakama ya nchi hiyo imemuamuru kulipa faini ya dola 20.

Serikali ya Zimbabwe ilipiga marufuku biashara ya uuzwaji wa bendera ya Taifa hilo bila kibali maalum kwa lengo la kupambana na kampeni iliyoanzishwa kwenye mtandao ya twitter iliyopewa hashtag ya #ThisFlag, ikiwahamasisha wananchi nchini humo kumiliki bendera zao ili wazitumie kwenye maandamano ya kuipinga Serikali.

Kampeni hiyo iliasisiwa na Mchungaji maarufu, Evan Mawarire aliyewataka Wazimbabwe kuvaa bendera hizo na kuwauliza maswali magumu maofisa wa Serikali.

Mwezi uliopita serikali ya Zimbabwe ilionya kwamba mtu yeyote atakayeagiza nje,kutengeza ama hata kuuza bendera ya taifa hilo bila rukhusa ama kuichoma mbali na kuiharibu atashtakiwa.

Waandamanaji wamekuwa wakitumia bendera za hizo wakati wa maandamano wakishinikiza Serikali hiyo inayoongozwa na Rais Robert Mugabe kujiondoa yenyewe kwa madai ya kushindwa kuwaletea maendeleo na kufanya ufisadi.

Iker Casillas apingana na waliotoa habari zake
Lucas Perez Kuongoza Mashambulizi Dhidi Ya Reading