Kidonda cha maumivu ya kuahirishwa ghafla kwa kilele cha Tamasha la Fiesta jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita, kimeacha kumbukumbu kwa waandaji wa tamasha hilo, Clouds FM ambao wanaitumiwa kama dongo somo kwa washindani wao ambao ni waandaji wa Wasafi Festival.

Leo, mtangazaji wa kipindi cha XXL cha Clouds Fm, Adam Mchomvu ametoa ushauri ambao unaonekana kuwa ni dongo, akiwataka wanaoanzisha matamasha na shughuli za burudani kama wao kujifunza kupitia waliyoyapitia badala ya kuwacheka wanapopata majanga.

“Clouds tumekuwa tunachonga barabara, kwahiyo inabidi kujifunza kwetu ili angalau uweze kufanya kitu. Ukiona Clouds hapa mjengoni kunawaka moto usikae huko unacheka [anaigiza sauti ya vicheko vya Diamond],” alisema Mchovu akipokea kijiti cha ushauri huo kutoka kwa B12.

Mtangazaji huyo ambaye alikuwa miongoni mwa watangazaji wa Clouds Fm walioonesha kwenye mitandao jinsi ambavyo waliumizwa na hawakuamini kama kilele cha Fiesta kimeahirishwa, alimaliza ushauri wake akisisitiza kuhusu mlengwa wake, “nadhani wametuelewa.”

Hii imetafsiriwa na wengi kama dongo kwa Wasafi kwa kuzingatia kuwa saa chache baada ya tangazo la kusitishwa kwa kilele cha Fiesta iliyokuwa ifanyike kwenye viwanja vya Leaders, Boss wa Wasafi, Diamond Platinumz aliweka picha kwenye Instagram akiangua kicheko, hali iliyosadikika kuwa akifurahia kwa kejeli kufungiwa kwa Fiesta.

Hata hivyo, mambo yaligeuka hivi karibuni baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kutangaza kulifungia tamasha la Wasafi kwa kukiuka masharti ya kibali chao, huku Fiesta iliyoahirishwa ikipangwa kufanyika Desemba 22 katika Viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam.

Uhasimu wa wazi kati ya Clouds Media Group kupitia Fiesta na Kampuni ya Wasafi kupitia Tamasha lao la Wasafi Festival ulishuhudiwa hivi karibuni, ambapo timu mbili za matamasha hayo zilionekana kurushiana vijembe huku baadhi ya wasanii nao wakijikuta wanaathiriwa na mgogoro wa pande hizo mbili.

Wasafi na Clouds Media Group ni watoto wa familia ya Mzee Joseph Kusaga ambao wanakabana mashati wakipimana nguvu kwenye ulingo wa biashara ya burudani.

Nilishaga sema siwezi kuhamia CCM- Kubenea
RC Gaguti atekeleza agizo la JPM

Comments

comments