Mchora katuni, Ramon Esono Ebale aliyekuwa anashikiliwa katika selo za polisi kutokana na michoro yake iliyotafsiriwa kuwa kichochezi dhidi ya Serikali ya Equatorial Guinea ameachiwa.

Akithibitisha kuachiwa kwa msanii huyo, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la EG Justice, Tutu Alicante aliiambia African Union kuwa Ebale alikuwa anafanya kazi iliyopaswa kufanywa na mashirika mengi yasiyo ya kiserikali ya nchi hiyo kuwawakilisha wananchi.

Ebale alikamatwa Septemba mwaka jana, lakini pamoja na mashtaka hayo Serikali ilieleza kuwa imemkuta na makosa ya utakatishaji fedha. Ilielezwa kuwa baada ya kufanya ukaguzi nyumbani kwake walikuta zaidi ya 1,500 euro zilizofichwa.

“Sifahamu chochote kuhusu fedha hizo. Ila najua wamenikamata kwa sababu ya katuni zangu ninazochora,” alisema Ebale alipokamatwa mwaka jana.

Shirika la EG Justice lililokuwa linamtetea lilidai kuwa kukamatwa kwake kuna uhusiano na katuni alizokuwa akichora kwenye kijitabu ‘Obi’s nightmare’ cha mwaka 2016 ambacho kilidaiwa kuelezea utawala wa Rais Teodoro Obiang Nguema.

Rais Obiang Nguema ameitawala nchi hiyo tangu mwaka 1979 alipoingia madarakani. Vyombo vya usalama nchini humo vimekanusha vikali madai hayo ya EG Justice.

Aveva alazwa ICU Muhimbili
Kumwezesha mwanamke kutainua uchumi wa Taifa