Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyita ameburuzwa mahakamani kwa makosa ya kuomba rushwa. uhujumu uchumi na kutakatisha fedha.

Leo, Agosti 9, 2019, Batanyita amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Kelvin Mhina wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka saba ikiwa ni pamoja na kuomba rushwa ya Shilingi milioni 200, kutakatisha fedha na uhujumu uchumi.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa kati ya Februari 9, 2019 na Februari 24, 2019, mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo. Katika kosa la kuomba rushwa, imeelezwa kuwa alitumia kofia ya kuwa mwajiriwa wa Takukuru kuomba rushwa ya shilingi milioni 200 kutoka kwa mfanyabiashara Hussein Gulamal ili aharibu ushahidi wa kesi ya kukwepa kodi iliyokuwa inamkabili mfanyabiashara huyo.

Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu na alirudishwa rumande kutokana na mashtaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.

Hakimu Mkazi Kelvin aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23, 2019.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 10, 2019
Mfumuko wa bei kwa mwezi julai 2019 wabaki asilimia 3.7