Mdahalo uliokuwa umeandaliwa na moja kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Kenya kwa ajili ya wagombea wenza wa nafasi ya urais umegeuka kaa la moto baada ya mgombea mmoja pekee kuhudhuria.

Mgombea aliyehudhuria katika mdahalo huo uliokuwa unarushwa moja kwa moja na kituo cha runinga nchini humo ni Muthiora Kariara (pichani) anayewania nafasi hiyo, akitarajia kuwa makamu wa rais endapo mgombea urais wa kujitegemea, Japheth Kaluyu atachagualiwa kuwa rais wa nchi hiyo.

Wagombea wenye ushindani mkubwa, Makamu wa Rais, William Ruto (Jubilee) na mgombea mwenza wa urais, Kalonzo Musyoka (Nasa) waliutosa mdahalo huo.

Hata hivyo, baadhi ya wagombea wa vyama vingine walifika wakiwa wamechelewa na kushindwa kuhudhuria mdahalo huo, huku wakiwatupia lawama waandaaji kwa kutowapa taarifa kwa usahihi na umakini.

Kariara alijibu maswali yote kwa muda wa saa moja, akitazamwa na wapiga kura wa nchi hiyo bila kupata upinzani kwenye mdahalo huo.

Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu, huku washindani wakuu wakiwa Rais Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa Nasa, uchaguzi unaotajwa kuwa wa ushindani zaidi katika historia ya chaguzi za nchi hiyo.

Video: Chadema yatoa tamko zito, TRA yamkana Ngeleja Escrow
Magazeti ya Tanzania leo Julai 18, 2017