Mapema leo alfajiri mdahalo wa pili wa mbio za Urais wa Marekani kati ya Donald Trump (Republican) na Hillary Clinton (Democratic) umevuta usikivu wa dunia, huku Trump akitishia kumfunga jela mpinzani wake huyo kama angekuwa Rais wa Marekani.

Bilionea huyo wa chama cha Republican ambaye muda mwingi aliutumia kumshambulia moja kwa moja Clinton, alidai kuwa kama kuna kitu ambacho mpinzani wake huyo angetakiwa kuwaomba radhi Wamarekani, ni kitendo cha kutumia barua pepe binafsi pamoja na kufuta maelfu ya barua pepe akiwa ofisini.

Alisema kuwa kwakuwa Clinton alifuta barua pepe 33,000 wakati uchunguzi ukiwa unaendelea, kama angekuwa Rais angekuwa ameshamfunga jela.

Aidha, Trump alisisitiza kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani atafungua mashtaka maalum dhidi ya Clinton ili kuhakikisha adhma yake hiyo inatimia.

“Kama nitashinda, nitaanzisha mashtaka maalum kwa ajili yako kuhusu maelfu ya barua pepe uliyoyafuta wakati yakiwa bado kwenye uchunguzi. Kama kuna kitu unachotakiwa kuomba msamaha wamarekani, ni hilo la kufuta barua pepe,” alisema Trump.

Akijibu madai hayo ya Trump, Bi. Clinton ambaye muda wote alionekana akiwa mtulivu licha ya kushambuliwa vikali na mpinzani wake, aliwaomba radhi Wamarekani kwa mara nyingine kuhusu sakata hilo la kufuta barua pepe lakini alidai kuwa tuhuma anazoziibua Trump sio za kweli na kwamba anajaribu kukwepa kuzungumzia suala la sera na kampeni kwa ujumla kwa sababu hata chama chake kinamtosa.

“lile lilikuwa kosa, na nimeomba radhi kwa suala hilo. Lakini kumekuwa na tuhuma za upotoshaji. Nilichukulia zile barua pepe za siri kwa umakini mkubwa. Hata baada ya uchunguzi ilibainika kuwa hakukuwa na barua pepe yoyote ambayo iliishia kwenye mikono isiyo salama,” alisema Clinton.

Katika hatua nyingine, Trump ambaye alifika katika mdahalo huo akiwa na wanawake ambao walidai kuwa Clinton aliwahi kuwadhalilisha, alimrushia makombora mengine mpinzani wake huyo akidai kuwa ingawa yeye ni mwanamke lakini amekuwa akiwashambulia wanawake wenzake.

Tuhuma hizo pia zilipingwa vikali na Clinton ambaye aliwakumbusha watu kuwa Trump amekuwa akiwashambulia wanawake muda wote akiwapa majina mabaya huku akitolea mifano ya walioumizwa na mashambulizi hayo.

Katika hatua nyingine, Trump aliendelea kumshambulia Clinton kuwa ndiye chanzo cha kukua kwa kundi linalojiita dola ya kiislam (ISIS) na kwamba Serikali ya Obama imeshindwa kulidhibiti na kuwalinda Wamarekani, madai ambayo pia yalipingwa vikali na Clinton.

Jicho la 3: Tukio la Mbeya litufumbue kumulika nidhamu shuleni, tusiishie kusikitika
Marekani Yaionya Saudi Arabia