Mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba wamekamiisha usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Uganda na klabu ya Gor Mahia FC ya Kenya, Meddie Kagere.

Taarifa zilizopatikana mchana huu zinadai kuwa, klabu ya Simba imekamilisha usajili wa mshambuliaji huyo aliyeng’ara wakati wa michuano ya Sport Pesa Super Cup iliyofanyika nchini Kenya, kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Kagere aliwasili jana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18, na kufanikiwa kufikia makubaliano.

Mshambuliaji huyo aliyewafunga Simba moja ya bao kati ya mawili katika mchezo wa fainali ya Sport Pesa Super Cup, amemalizana na uongozi wa klabu hiyo mpya akiwa chini ya wakala wake, Patrick Gakumba.

Kagere ameungana na beki kutoka Ivory Coast, Pascal Wawa ambaye naye imeelezwa tayari ameshamalizana na Simba, japo bado haijathibitishwa rasmi kama ameshasaini mkataba.

Ujio wa Kagere unaweka wasiwasi nafasi ya mshambuliaji kutoka nchini Burundi Laudit Mavugo, ambaye hapewi nafasi kubwa ya kuendelea kusalia katika kikosi cha Simba kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Jeshi la polisi lasitisha maombi ya ajira
Radja Nainggolan atua rasmi Inter Milan