Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe amedai kuwa baraza la mawaziri aliloliunda Rais John Magufuli halijapunguza gharama za matumizi ya fedha za serikali kama ilivyodaiwa huku akikosoa pia sera ya kudhibiti safari za nje.

Membe ameeleza kuwa kiuhalisia rais Magufuli hakupunguza baraza la mawaziri kama ilivyodaiwa bali alichokifanya nikubadili mifuko (wizara) iliyobeba jumla ya idadi sawa ya mayai (mawaziri).

“Alichokifanya ni sawa na kuwa na mayi kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,

“Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa atakuwa hajapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai,” Membe ananukuliwa na gazeti la Mwananchi.

“Maana yake ni kwamba ameendeleza wizara zilezile, lakini akaamua kuzikusanya pamoja. Hiyo haimaanishi kuwa atakuwa amepunguza gharama za uendeshaji wake,” alieleza.

Kauli ya Membe inaungana na kauli ya aliyekuwa naibu waziri wa kazi na ajira, Dk. Makongoro Mahanga aliyehamia Chadema, aliyesema kuwa rais Magufuli hakupunguza gharama kiuhalisia kwa kuzingatia idadi kubwa ya makatibu wakuu na manaibu wao aliowateua.

Kuhusu safari za nje, Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ameeleza kuwa rais Magufuli lazima atafanya safari za nje kutokana na hali halisi huku akisisitiza kuwa endapo atajitenga kwa kujifungia nchini lazima nchi nyingine pia zitamtenga.

“Tanzania sio kisiwa. Hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako. Lazima utakewnda mwenyewe au Waziri wa Mambo ya Nje kwa sababu kuna vikao nje ya nchi ambavyo mabalozi hawaruhusiwi kuingia. Ukijaribu kujifanya kisiwa utakuwa kama Zimbabwe. If you isolate yourself, you will be isolated (ukijitenga, utatengwa).”

Alisisitiza kuwa lazima waziri wa mambo ya nje ya nchi awe nje kwa muda mwingi na ikitokea yuko ndani ya nchi kwa muda wa mwezi mmoja mfululizo, lazima ni mgonjwa.

Chanzo: Mwananchi

Kranevitter Azigonganisha Chalsea Na Arsenal Mjini Madrid
Gundogan Kumfuata Jurgen Klopp Liverpool