Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa wa serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe amezungumzia mpango wa kustaafu siasa kama walivyofanya wanasiasa wakongwe, Samwel Sitta na Dk. Wilbroad Slaa.

Hivi karibuni Membe amekuwa akishambuliwa na makada wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufuatia kauli zake za kuikosoa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Membe ameeleza kuwa hana mpango wa kustaafu siasa kwa kuwa anafahamu siasa haina mwisho, bali ataanza kujikita katika uandishi wa vitabu vinavyohusu mambo mbalimbali ya dunia aliyoyashuhudia na kuyasoma kwenye vitabu vingine.

“Tafsiri ya siasa ni mchakato wa namna ya kuyashughulikia matatizo ya watu. Usipoyashughulikia vizuri utabadilisha siasa kutoka kwenye amani kwenda kwenye machafuko,” Membe alilieleza gazeti la Mwananchi.

“Hilo la kuandika vitabu nimeshalianza, nina vitabu zaidi ya 265 nimevisona na kuvihifadhi katika maktaba yangu kuhusu mambo mbalimbali ya dunia. Na mimi ninatengeneza vinne, muda ukifika nitatoa taarifa,” aliongeza

Alieleza kuwa kati ya vitabu hivyo, kimoja kinahusu maisha yake akiwa kama mwanasiasa aliyedumu kwenye tasnia ya siasa kwa miaka 35.

Raphael Kiongera: Kwa Sasa Ninamuachia Mungu
Idris aweka wazi mwezi ambao yeye na Wema wanatarajia kupata mtoto