Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Bernard Membe amesema kuwa watashinda kwa kishindo cha vumbi kwenye uchaguzi mkuu Oktoba, 2020.

Akizungumza mkoani Lindi, Membe amewahakikishia ushindi huo wafuasi wa chama hicho baada ya kuzindua Ilani yao na kueleza kuwa ni ilani inayokubalika kwa urahisi kwa wananchi.

Mwanasiasa huyo mkongwe pia ameeleza kuwa yeye na mgombea mwenza wake watakuwa mshumaa wanapoinadi Ilani ya chama hicho kote nchini na wananchi ndio watakaoamua.

“Sisi ndio tutakuwa mishumaa ya ACT, tutatembea kote nchini kuiuza na kuinadi ilani yetu na msikilize siku ya Oktoba 28 kivumbi… hakuna cha kutuibia, hakuna cha ku-test mitambo. Ushindi huu utaamliwa na the will of the people (matakwa ya wananchi), sio matakwa ya watawala,” amesema Membe.

Katika hatua nyingine, Membe ameeleza kuwa moja kati ya mambo watakayoifanyia kazi kwa kina na kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia.

Alikosoa mchakato wa kupitisha wagombea ubunge kwa upande wa wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) akidai kuwa kimekosa kuangalia usawa wa kijinsia.

“Binti anaacha ubunge wa viti maalum anapata jimbo halafu wewe unamuondoa? Ndio maana sisi tutajali usawa wa kijinsia. Wewe dada ukienda kwenye jimbo ukapigania ukashinda, tena ukawa wa kwanza, hata iweje utarudi bungeni tu,” amesema Membe.

Membe alijiunga na ACT-Wazalendo na kupewa nafasi ya kugombea urais, baada ya kufukuzwa CCM kwa sababu za kinidhamu.

Jeshi la Mali lafanya uteuzi
JPM: Nataka kwenda mbinguni, wanipe uwaziri wa Malaika