Mshambuliaji kutoka nchini Uholanzi, Memphis Depay ameshindwa kujizuia na kujikuta akirejesha madongo kwa mashabiki wanaombeza katika kipindi hiki.

Depay, amefanya hivyo baada ya kushambuliwa kwa muda mrefu na wanaochukizwa na mwenendo wake kwenye kikosi cha Man Utd ambacho kilionyesha mategemeo makubwa kwake, tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu.

Depay, amesema yanayozungumzwa dhidi yake ameyasikia na hana budi kufanya juhudi ili kuwanyamazisha wanaombeza kwa kumuita bitozi ambaye hana msaada kwenye kikosi cha mashetani wekundu.

Amesema kilicho mbele yake ni kuhakikisha Man Utd inafikia malengo yake kwa msimu huu, na haoni sababu ya watu kumzungumzia vibaya ili hali msimu wa ligi bado unaendelea.

Kejeli kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, zilianza kupewa nafasi kubwa miongoni mwa mashabiki wa Man Utd pamoja na wale wa klabu nyingine nchini humo, mwezi uliopita ambapo kasi yake ya upachikaji mabao pamoja na kutoa msaada kwa wenzake ilipoanza kuonekana inapungua.

Depay, alisajiliwa na Man Utd, kwa ada ya uhamisho wa pauni, million 25, akitokea nchini kwao Uholanzi, alipokua akiitumikia klabu ya PSV Eindhoven ambapo kwa msimu wa 2014/15 aliifungiwa mabao 22.

Katibu UVCCM Wilaya Ateuliwa Kuwa Mbunge Viti Maalum Chadema
Sergio Ramos Kufanyiwa Upasuaji Wa Bega