Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amemtaka Meneja wa TANESCO Wilaya ya Biharamulo, Ernest Milyango kuandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo nchini, Dkt. Tito Mwinuka  kueleza sababu zinazopelekea kukatika hovyo kwa umeme wilayani humo.

Byabato ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo baada ya kupokea taarifa ya hali ya umeme kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Kanali Mathias Kahabi, ambaye ameeleza kuwepo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani humo ambayo imekuwa kero sugu.

Ziara hiyo ya kutembelea kituo cha kupozea umeme kinachojengwa Nyakanazi wilayani humo ni ufuatiliaji wa maelekezo ya Waziri wa Wizara hiyo, Medard Kalemani ambayo aliyatoa wakati wa ziara yake mwezi Desemba mwaka Jana.

“Ninachojua umeme hapa nchini tunao umeme wa kutosha hivyo hatutarajii kuwa na sababu zisizo za msingi zinazopelekea kukatika kwa umeme hasa kwa Wilaya hii ambayo tayari ipo kwenye gridi ya Taifa, bahati nzuri nimekuja na mkurugenzi mtendaji wa TANESCO naelekeza kufika mwishoni mwa wiki ijayo nipate barua ya kuonyesha sababu za kitaalamu kuhusu suala hili,” amesema Byabato.

Akijibu kuhusu changamoto ya wananchi kupewa bei mkanganyiko za uunganishwaji wa umeme tofauti na maelekezo ya Serikali, Byabato amewaelekeza wataalamu wote wa TANESCO NA REA nchini kuwa bei ya uunganishaji wa umeme kwa wananchi walioko vijijini ni shilingi elfu 27,000/= tu na si vinginevyo, na kuongeza kuwa umeme unatakiwa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao.

Aidha Byabato ameeleza kuwa kituo hicho ni kitovu cha umeme kwa Mkoa wa Kagera hivyo ukamilishwaji wake unatakiwa kwenda sambamba  na ujenzi wa njia za kusafirishia umeme kwenda kwa wananchi ambapo itawezesha Mkoa mzima kuanza kutumia umeme wa Grid ya Taifa na kuachana na umeme tegemezi.

Kituo cha kupozea umeme Nyakanazi kinajengwa na  kampuni ya LARSEN & TURBO COP. LTD ya nchini India kwa gharama ya zaidi shilingi bilioni 22, na kinatarajiwa kukamilika kufikia Machi 31 mwaka huu.

Simba SC yamtambulisha kocha wake mpya
Mlinzi aliyepiga hospitalini aondolewa