Lionel Messi usiku wa kuamkia leo aliingia kwenye katika vitabu vya kihistoria kwa mara nyingine tena, ambapo safari hii ametinga kwenye kundi la nyota wa soka duniani waliowahi kufunga mabao zaidi ya 700.

Messi aliingia kwenye historia hiyo, kwa kufunga bao la mkwaju wa penati dhidi ya Atletico Madrid kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), huku FC Barcelona wakilazimishwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Kabla ya bao hilo Nahodha na Mshambuliaji huyo wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentina alikuwa amepachika jumla ya mabao 699.

Mara baada ya mchezo huo dhidi ya Atletico Madrid, Messi aliongeza idadi ya wachezaji waliofunga idadi hiyo ya mabao kutoka saba (7) na kufikia nane (8) wakiongozwa na nyota wa zamani wa timu za Taifa za Austria na Czechoslovak, Josef Biscan anayeshikilia rekodi ya kufunga idadi kubwa ya mabao katika mashindano rasmi, akifumania nyavu mara 805.

Lilikuwa ni bao ambalo sio tu lilimfanya Messi aingie katika vitabu vya kumbukumbu, bali pia lilivutia wengi kutokana na ufundi ambao Mshambuliaji huyo aliutumia katika kupiga penati hiyo ambapo aliikwamisha kimiani kwa staili ya kubetua mpira na kuuelekeza mahali karibu na aliposimama kipa (Panenka).

FC Barcelona walipata penati hiyo baada ya beki wao Nelson Semedo kufanyiwa madhambi na Luiz Felipe ndani ya eneo la hatari la Atletico Madrid.

Messi anakuwa mchezaji wa pili wa kizazi cha sasa kufikisha idadi hiyo ya mabao mwingine akiwa ni mpinzani wake, Cristiano Ronaldo ambaye amefumania nyavu mara 725.

Wengine waliofikisha ama kuvuka mabao 700 ni Romario aliyepachika mabao 772, Pele (767), Ferenc Puskas (746), Gerd Muller (735) na Ronaldo De Lima aliyefunga mabao 725.

Hata hivyo bao hilo la Messi halikutosha kuifanya FC Barcelona iibuke na ushindi katika mchezo huo na kujikuta ikilazimishwa sare ya mabao 2-2 ambayo imezidi kuwaweja kwenye mazingira magumu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania msimu huu.

Saul Niguez aliisawazishia Atletico Madrid katika dakika ya 62 kwa mkwaju wa penati na kuifanya imalizike kwa sare hiyo baada ya Diego Costa kuizawadia FC Barcelona bao la kwanza kwa kujifunga wakati upande wa Atletico Madrid bao lao la kwanza likipachikwa na Niguez kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 15.

Matokeo hayo yameifanya FC Barcelona kufikisha alama 70 na kuwa nyuma ya vinara Real Madrid kwa tofauti wa alama moja.

Hata hivyo, Real Madrid wana mchezo mmoja mkononi na kesho watacheza dhidi ya Getafe na ikiwa watashinda, wataongeza pengo la alama kufikia nne (4).

Michezo Mingine Ya Ligi kuu Ya Hispania Kuanzia leo Julai Mosi
Naibu waziri amsimamisha kazi ofisa madini Tunduru
Mingange: Simba SC walistahili ubingwa

Comments

comments