Kiungo kutoka nchini Ujerumani, Mesut Ozil amewataka wachezaji wenzake wa klabu ya Arsenal kupambana hadi katika hatua za mwisho, endapo wanahitaji kurejesha imani kwa mashabiki katika suala la kuwania ubingwa wa ligi ya England msimu huu.

Ozil, ametoa rai hiyo kwa wachezaji wenzake kutokana na dharau iliyojengeka kwa Arsenal katika kipindi hiki, ambacho imeonekana huenda wakashindwa kuonyesha upinzani wa dhati dhidi ya Leicester City, wanaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya point 11 dhidi ya The Gunners wanaoshika nafasi ya tatu.

Ozil amesema ni vigumu kwa shabiki wa soka kumuelewa ama kukubaliana na rai aliyoitoa kwa wachezaji wenzake, lakini kwake upande wake anaamini katika soka chochote kinaweza kutokea na ulimwengu ukashangaa.

Amesema, kila mchezaji wa Arsenal anapaswa kujihisi aibu katika harakati walizonao kwa sasa, hasa ikizingatiwa klabu hiyo imekaa zaidi ya miaka 10 bila kushinda taji la ubingwa wa nchini England.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, amesema atakuwa wa mwisho kuamini kama wameshindwa kupambana katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu, huku michezo zaidi ya saba ikisalia na wana uwezo wa kuzifunga timu pinzani.

Ozil, ametoa msukumo huo kwa wachezaji wenzake, huku kikosi cha Arsenal kikiwa katika maandalizi ya mwisho kuelekea katika mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England utakaounguruma kwenye uwanja wa Emirates dhidi ya Watford, hapo kesho.

Watford, watafunga safari kuelekea kaskazini mwa jijini London, huku wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja katika uwanja wa Emirates kwenye wa hatua ya robo fainali wa michuano ya kombe la FA majuma matatu yaliyopita.

Kamati Ya Nidhamu Ya Tff Kukutana Kesho
Slaven Bilic Amtabiria Makubwa Dimitri Payet