Rais wa Mexico, Andres Manuel Lopez ametangaza kupiga mnada ndege ya Rais na kwamba fedha zitakazopatikana zitatumika kusaidia jitihada za kudhibiti uhamiaji haramu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mexico na Marekani kufikia makubaliano ili kuepuka vikwazo vya kiuchumi na ongezeko la kodi katika biashara ya nchi hizo mbili. Mexico iliahidi kuongeza vikosi mipakani kudhibiti wahamiaji haramu kwenda Marekani.

Hata hivyo, uamuzi wa kuuza ndege ya Rais ni sehemu ya ahadi ya kiongozi huyo wakati wa kampeni ambapo alisema fedha zitakazotokana na mauzo hayo zitatumika kusaidia jamii masikini zaidi.

Ndege hiyo aina ya Boeing 787 Dreamliner ilinunuliwa mwaka 2016 kwa $218 milioni lakini sasa inaweza kuuzwa kwa kiasi kisichopungua $150 milioni.

Rais Lopez alitekeleza ahadi yake siku chache tu baada ya kuingia madarakani. Ndege hiyo imeanza kupigwa mnada miezi michache iliyopita ikiwa California, Marekani.

Ameeleza kuwa sehemu ya fedha zitakazopatikana zitatumika kupeleka vikosi vya wanajeshi 60,000 mpakani kwa ajili ya kusaidia kudhibiti uhamiaji haramu.

“Kuhusu ni kiasi gani huu mpango [wa kupeleka vikosi mipakani] utagharimu, ngoja niwaeleze tu kuwa tuna bajeti. Fedha zitapatikana kupitia mauzo ya ndege ya Rais,” alisema Rais Lopez Obrador alipozungumza na waandishi wa habari.

Mexico pia ina mpango wa kuuza ndege 60 za Serikai pamoja na helicopter 70.

Rais wa Marekani, Donald Trump aliahidi kwenye kampeni yake kuwa atajenga ukuta kati ya Marekani na Mexico ili kudhibiti uhamiaji haramu, lakini Bunge la nchi yake limekataa kupitisha bajeti kutekeleza nia hiyo.

 

Video: Zitto azuiwa kusafiri nje ya nchi, Macho, Masikio Bajeti kuu leo
Mwanafunzi aliyeruka ukuta wa Ikulu na kisu alianika mpango wake Facebook

Comments

comments