Kikosi cha Kagera Sugar kimekamilisha maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utawakutanisha dhidi ya Young African kesho Jumatano (Februari 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salam.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Mecky Mexime, kikosi cha klabu hiyo ambacho tayari kimeshawasili jijini Dar es salaam, kimekamilisha maandalizi ya kuelekea mchezo huo ambao Young Africans watakua nyumbani.

Kocha Mexime amesema wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo,ambao wanahitaji kushinda na kuondoka katika uwanja wa ugenini wakiwa na alama tatu muhimu.

Amesema anatambua mchezo utakua na upinzani mkali kutokana na wapinzani wao kuwa katika kiwango kizuri, lakini amekiandaa kikosi chake kikamilifu ili kufikia lengo walilojiwekea hiyo kesho.

Amesema pamoja na kujiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Young Africans, kikosi chake pia kimejiandaa na michezo mingineya mzunguuko wa pili ambao ni lala salama kwa msimu huu 2020/21.

“Kwenye michezo yetu yote ndani ya uwanja  tumejipanga kuona kwamba tunapata pointi tatu muhimu hivyo mchezo wetu ujao dhidi ya Yanga nao ni sehemu ya mchezo, tutaingia kwa kuwaheshimu ila tunazihitaji pointi tatu.”

“Mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti kwani ushindani ni mkubwa na wapinzani wetu nao sisi tunawaheshimu hivyo.” Amesema Mexime

Katika mchezo uliopita Kagera Sugar, waliambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Gwambina FC, Uwanja wa Kaitaba inakutana na Young Africans iliyotoka kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Sokoine.

Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliozikutanisha timu hizo Uwnaja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera, Young Africans iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tonombe.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans wameendelea kuwa kileleni kwa kufikisha alama 45, huku Kagera Sugar wakishika nafasi ya 10 wakiwa na alama 23, zote zimecheza jumla ya mechi 19.

Simba SC kuanza safari ya Musoma, Mara
Namungo FC: Tumenyanyaswa bila hatia