Kocha mkuu wa timu ya Kagera Sugar, Meck Mexime amewashangaa baadhi ya mashabiki wa klabu ya Simba na Young Africans ambao wamekuwa wakimnasabisha na miamba hiyo ya soka nchini kila anapo wafunga.

Mexime amesema wakati akiwa na timu ya Mtibwa Sugar alikuwa na bahati ya kuifunga Young Africans na alisababisha makocha Ernest Brandt na Tom Saintfet kufukuzwa kazi baada ya kuwafunga katika uwanja wa Jamhuri hali iliyomfanya kuchukiwa na mashabiki wa timu hiyo wakimtuhumu kuwa ni Simba.

Kocha huyo ameendelea kusema baada ya kujiunga na Kagera amekuwa akiwafunga Simba ambao wanaonekana kuwa bora ikiwemo mchezo walioshinda mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli misimu miwili iliyopita na kushushiwa lawama kuwa ni Young Africans.

Mexime amesema anapenda kuzifunga timu hizo kwa kuwa zinawekeza sana kwa kuleta makocha na wachezaji kutoka nje hivyo anawakumbusha kuwa hata hapa ndani kuna makocha wazuri na wachezaji pia.

“Yaani kwenye soka la Tanzania timu ni mbili tu Simba na Yanga. Ukiifunga Simba unaambiwa wewe Yanga, ukiifunga Yanga unaambiwa ni Simba.”

“Wakati nikiwa Mtibwa nilikuwa na bahati sana ya kuifunga Yanga nikatukanwa sana na mashabiki kuwa mimi ni Simba, lakini kwa sasa nipo Kagera naifunga Simba mara kwa mara naambiwa mimi ni Yanga kwa hiyo nimeshazoea nafanya kazi yangu tu,” alisema Mexime.

CORONA: Champions League, Europa League bado hali tete
CORONA: Mwanasiasa ajitetea kumtusi Ronaldo

Comments

comments