Wakati sakata la mishahara kwa watumishi hewa likiendelea, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob amebaini kuwepo harufu ya ufisadi katika manispaa yake unaoonesha ukarabati wa barabara uliotumia shilingi milioni 392 ambao haukufanyika.

Taarifa ya bajeti ya ununuzi ya Manispaa hiyo ilionesha kuwa fedha hizo zilitumika kukarabati barabara ya Sinza-Igesa kuanzia Januari hadi machi mwaka huu lakini baada ya kutembelea na kukagua eneo la barabara hiyo, walibaini kuwa hakuna kilichofanyika lakini fedha  hizo zililipwa kwa mkandarasi, Skol Buiding Contract Lt.

“Hivi, kama tungenyamaza tusiamue kukagua miradi hii, nani angesimama kueleza hayo. Mnaleta hadithi wakati tayari mmeshalidanganya Baraza la Madiwani kwamba fedha hizi zimetumika kukarabati barabara hii?” alihoji Meya.

Aliwataka Takukuru kuingilia kati na kuchukua hatua stahiki na pia wote waliohusika kuandaa taarifa hiyo ya matumizi ya fedha hizo ambayo sio ya kweli.

Mchumi wa Manispaa hiyo, Huruma Eugen alisema kuwa fedha hizo zilizoonekana katika taarifa hiyo zilitumika kulipa madeni ya nyuma kwa wakandarasi, majibu ambayo hayakuonekana kumridhisha Meya na Madiwani wa Manispaa hiyo.

Meya alisisitiza kuwa kama fedha hizo zilitumika kulipa madeni ya nyuma zilipaswa kuonesha hivyo kwenye taarifa hiyo na sio kueleza kuwa zilikarabati barabara hiyo.

 

Kikosi Cha Misri Kitakachoivaa Taifa Stars Chatajwa
Mbunge wa CCM ahoji kwanini Mwijage, Mwigulu wasitumbuliwe Jipu