Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema kuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe alikamatwa jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kukutwa akipokea rushwa.

Hapi ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo ameeleza kuwa Meya huyo alikamatwa na maafisa wa Takukuru katika Hoteli ya Gentle Hills.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Takukuru waliweka mtego na kumnasa Kimbe akiwa anapokea rushwa kutoka kwa mzabuni aliyepewa kazi ya kukusanya ushuru katika Manispaa hiyo.

“Meya alikamatwa majira ya saa 11 jioni katika Hoteli ya Gentle Hills, akipokea rushwa kutoka kwa mkurugenzi wa Gracious kwa ahadi ya kumpa zabuni ya ujenzi na kukatisha ushuru,” alisema Hapi.

Aidha, alisema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu tabia za baadhi ya watu wenye mamlaka wakiwemo madiwani kuomba rushwa, hali inayominya haki zao.

Takukuru na jeshi la polisi hawajatoa taarifa ya kina kuhusu kumshikilia Kimbe, ambaye kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa Hapi atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Manispaa hiyo inaongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, chini ya Meya huyo.

Magunia 17 ya Bangi yakamatwa mkoani Pwani
Serikali yafunga makanisa 34 kwa 'Oparesheni Okoa'