Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire (CCM) amelazimika kukimbia ofisi yake baada ya mashine inayotumika kutoa hewa safi (AC) ndani ya ofisi hiyo kutoa hewa inayosadikika kuwa na sumu.

Meya huyo amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo limetokea ikiwa ni mara ya pili katika ofisi yake ambapo awali alilazimika kulazwa katika hospitali moja jijini Nairobi kutokana kuvuta hewa kama hiyo ndani ya ofisi hiyo.

Alisema mara baada ya kurejea kutoka Nairobi kupata matibabu, aliamua kurudi na kuendelea na shughuli zake lakini alipoingia kwenye ofisi hizo kwa mara nyingine tukio hilo lilijirudia.

Kutokana na tukio hilo, wanachama wa CCM kata ya Mahina wameandamana hadi katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupinga vitendo vya kutishiwa maisha kwa diwani wao, huku wakiwanyooshea vidole viongozi wa ngazi za juu wa Halmashauri hiyo kwa kile walichodai wameshindwa kuchukua hatua stahiki.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema kuwa Jeshi lake halikupokea taarifa za Meya huyo kutishiwa maisha bali limepokea taarifa za kuwepo hewa chafu inayoaminika kuwa ni sumu ndani ya ofisi yake na inalifanyia kazi jambo hilo.

“Hatujapata malalamiko kutoka kwake huenda anatafutwa auawe, au wenda anahitaji ulinzi maisha yake yako hatarini… malalamiko yaliyokuja ni kwamba ame- abandon ofisi kwa sababu baada ya AC kuwa imewasha harufu aliyoisikia kuwa sio ya kawaida,” alisema.

Alisema kuwa Mkemia wa Serikali na Jeshi la Polisi wamechukua sampuli ya hewa hiyo kwa ajili ya uchunguzi ili waweze kubaini kama ni sumu au vinginevyo.

Kila aliyeingia kwenye ofisi hiyo mbele ya waandishi wa habari ndani ya muda mfupi alitoka akipiga chafya.

Ulimwengu aponda hali ya Demokrasia nchini, Kinana ataka viongozi waombe radhi
Ayler afungukia maisha yake ya IFM.