Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob (Chadema) amevutana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda akimtuhumu kuingilia kazi za Halmashauri hiyo zilizo nje ya mipaka yake.

Meya huyo amepinga vikali hatua ya Paul Makonda kutangaza hadharani taarifa za kamati ya mipango na fedha ya Manispaa hiyo akieleza kuwa inatarajia kupokea zaidi ya dola milioni 300 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 600 kutoka katika Benki ya Dunia.

Jacob alieleza kuwa Makonda hakuwa na mamlaka ya kutoa taarifa hizo kwani hata kwenye kikao cha kamati hiyo hakuhudhuria, hivyo ameamua kuonya muingiliano huo wa mipaka ya majukumu mapema ili shida kubwa zaidi isitokee siku za usoni.

“Vikao hivyo vya Halmashauri ni siri, kwahiyo huo ni upotoshaji wa Makona,” alisema. “Mimi nalalamikiwa na wajumbe wa kamati, wanasema kwa nini taarifa za kikao ambazo ni za siri zinatangazwa wakati bado michakato yake inaendelea?” alihoji.

Jacob alidai kuwa Mkuu huyo wa wilaya amekuwa akiingilia mara kwa mara majukumu yanayopaswa kufanywa na Mkurugenzi au Meya wa Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa ahadi ambazo msingi wake ni vikao vya halmashauri hiyo.

Alionya kuwa endapo ataendelea kutoa taarifa hizo, Halmashauri hiyo itawazuia maafisa Tarafa kuingia kwenye vikao.

Hata hivyo, Makonda alipoulizwa kuhusu madai ya Meya huyo alisema hawezi kuzumgumzia suala hilo kwani Meya huyo bado anajifunza kazi kwa kuwa alichaguliwa hivi karibuni. Alisema kuwa baada ya kujifunza na kuelewa hatakuwa na malalamiko kama hayo.

Museveni aeleza sababu za kumfungia nyumbani Dk. Besigye, mpango wa kuachia madaraka
Ne-Yo afunga ndoa na mrembo huyu