Na: Joseph Muhozi (Josefly)

Wiki hii nchi kadhaa za Afrika, zitampokea mgeni, Makamu wa Rais wa Marekani, Wakili Msomi, Bi. Kamala Harris. Mgeni wetu ataingia Tanzania Machi 29, 2023 akitokea nchini Ghana ugeni ambao kwa Tanzania utakuwa ugeni wa aina yake na wenye muonekano tofauti kabisa na itakavyokuwa kwa nchi nyingine.

Hii ni kwa sababu yatakutana majembe, Wanawake wawili wenye vyeo vya juu zaidi nchini kwao. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan a.k.a Mama wa Taifa aliyeweka historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke Afrika Mashariki na Harris ambaye ndiye mwanamke wa kwanza kushika cheo cha juu zaidi nchini Marekani katika historia ya nchi hiyo.

Kwa ufupi itakuwa ‘majembe wawili wanawake walioandika historia nzito’. Hata hivyo, haitakuwa mara ya kwanza. Viongozi hawa walikutana na kufanya mazungumzo Aprili 2022, Ikulu ya Marekani. Na sasa itakuwa zamu ya kukamilisha walichozungumza, na watakuwa Ikulu ya Magogoni, Bandari Salama.

Makamu wa Rais wa Marekani, Wakili Msomi, Bi. Kamala Harris. Picha ya US Embassy.

Bi. Harris ataandika historia pia ya kukanyaga ardhi yenye mlima mrefu zaidi barani Afrika, ardhi yenye Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ambayo ni miongoni mwa maajabu kumi ya asili ya dunia, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, sio hivyo tu, atakuwa mwenye bahati kukaa kwenye ardhi ya nchi yenye amani zaidi Afrika Mashariki na kati.

Ataitwa mwenye bahati ya kukutana na wananchi wastaarabu zaidi, wakaazi wa Pwani ya Afrika Mashariki. Na kama aliwahi kusimuliwa na watangulizi wake, viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani waliowahi kubahatika kufika Tanzania, nikiwataja majina na kofia walizokuja nazo kwenye mabano Bill Clinton (Rais wa Marekani), Barack Obama (Rais wa Marekani) na Hillary Clinton (Waziri wa Mambo ya Nje), sasa itakuwa zamu yake.

Tayari Bi. Harris ameshachagua ngoma atakazosikiliza atakapokuwa njiani na atakapokuwa Tanzania, ambazo ni pamoja na Single Again ya Konde Boy, Harmonize, Utaniua ya Zuchu, Mahaba ya Alikiba na Jux pia. Hawa ni wasanii wa Bongo ambao amechagua kuwasikiliza kwenye safari yake kuelekea Tanzania, kwa mujibu wa taarifa aliyoiweka kwenye akaunti yake rasmi ya Twitter na uhalisia ni ndiyo, waamba ngoma tumeivuta kwetu, sasa tuendelee.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris (kulia) na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Picha ya Ubalozi wa Tanzania Washington DC, Marekani.

Je, huyu mgeni wetu ni nani hasa?

Kamala ni Makamu wa Rais wa 49 katika historia ya Marekani, na ndiye mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu zaidi baada ya Rais kama nilivyoeleza awali. Ni wakili msomi na nguli, Mama mwenye umri wa miaka 58, mwenye asili ya bara Asia na Afrika, aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo kupitia Chama cha Democratic, Januari 20, 2021. Ndiye mwanamke wa kwanza mwenye asili ya bara la Asia kushika nafasi hiyo, kama ilivyokuwa kwa Barack Obama kuwa Rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika.

Mama yake ni Shyamala Gopalan, mtaalam wa Bailojia kutoka India. Mama huyo aliingia Marekani mwaka 1958 akitokea India kwa ajili ya kusoma Chuo Kikuu. Hapo alikutana na Bw. Donald Harris, Mmarekani mwenye asili ya Jamaica. Bw. Donald Harris alikuwa Profesa wa Chuo Kikuu,aliyeingia Marekani mwaka 1961 akitokea Jamaica. Wasomi hao wakaungana, akapatikana mtoto waliyempa jina la Kamala, mwaka 1964.

Bi. Harris amewahi kunyanyaswa na kubaguliwa kwa sababu ya ngozi yake. Katika moja ya mahojiano yake, alisema baada ya wazazi wake kuvunja ndoa (kuachana) akiwa na umri wa miaka saba, siku za wikendi yeye na dada yake walikuwa wanamtembelea baba yao aliyekuwa anaishi Palo Alto. Anasema Watoto wa jirani walikatazwa kucheza nao kwakuwa wao ni weusi.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris (kulia) akiwa na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo. Picha ya Twitter.

Ukifahamu kilichomsukuma kuwa mwanasheria, kinasikitisha. Na huenda hiki ndicho chanzo cha yeye kukomaa na sheria na kuwakomalia wenye kesi za unyanyasaji wa kingono.

Wanda Kagan, rafiki wa Bi. Harris tangu alipokuwa shuleni, aliiambia CBC News mwaka 2020 jinsi alivyomweleza Bi. Harris kuwa anaingiliwa kingono na baba yake wa kambo. Kagan anasema kuwa Bi. Harris alimwambia mama yake ambaye alifanya uamuzi wa kumchukua Kagan ili waishi pamoja kuepuka ukatili huo na anasema kuwa kitendo hicho ndicho kilimpa nguvu zaidi Bi. Harris kujiimarisha katika masomo ya sheria na kutetea wanawake na watoto kama wakili.

Awali, mwaka 1986, Bi. Harris alijiunga na Chuo Kikuu cha Howard cha Washington akachukua Shahada ya Sayansi ya Siasa na Uchumi. Kisha, akaamua kurudi Chuo Kikuu tena kuchukua masomo ya sheria ambayo alibobea na mapambano yakaendelea.

Bi. Harris ni wakili mwenye wasifu mzito. Alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Jimbo la California, na huko alifahamika kama wakili mwenye msimamo na shupavu, tangu mwaka 2011 hadi 2017. Baadaye, alichaguliwa kuwa Seneta wa California mwaka 2017 hadi 2021. Alihangaika na California, sehemu ambayo alizaliwa na akatoboa. Kwa Bi. Harris ule msemo wa ‘nabii hakubaliki kwao’ ulimpita kando.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris. Picha ya Reuters.

Hata hivyo, Bi. Harris alipanda ngazi akitokea chini sana. Juhudi, maarifa na hekaheka ndizo zilizomjenga hadi kufikia hatua hiyo, alisoma katika Chuo Kikuu cha Howard na baadaye Chuo Kikuu cha California Shule ya Sheria Hastings, alikochukulia masomo yake ya sheria. Alipohitimu, alianzia chini kama Afisa wa kawaida. Mwanzo mnyenyekevu. Alianza kama Afisa Sheria katika Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya/Kaunti ya Alameda. Na baadaye alipanda na kuwa Afisa katika Ofisi ya Mwanasheria wa Jiji la San Francisco.

Tangu alipogusa kwenye ofisi hiyo na kupiga kazi, umahiri wake ukaiwasha nyota iliyo ndani yake. Akaanza kupaa taratibu kuelekea kule ambako Mwenyezi Mungu alipanga awepo, akiweka juhudi, nidhamu na maarifa.

Mwaka 2003 alichaguliwa kuwa Mwanasheria wa Wilaya ya San Francisco. Mwaka 2010 nyota iliwaka zaidi, akachaguliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa California, akapiga kazi vizuri akakubalika. Wakili Msomi, Harris akachaguliwa tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa California mwaka 2014.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris. Picha ya Anadolu Agency.

Bi. Harris alicheza karata zake vizuri, akaendelea kukubalika. Mwaka 2016 alimshinda nguli wa siasa Loretta Sanchez, akachaguliwa kuwa Seneta, akaandika historia ya kuwa mwanamke wa pili mwenye asili ya Afrika kuwa Seneta wa Marekani, na mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Bara la Asia kuwa Seneta wa Marekani.

Bi. Harris aliyagusa masikio ya Wamarekani wengi, kwa jinsi alivyokuwa akiwahoji maafisa wa utawala wa Rais Donald Trump wakati wa Bunge la Seneti, hususan jinsi alivyomkalia kooni kwa maswali mazito mteule wa Trump wa Mahakama ya Juu, Brett Kavanaugh aliyekuwa anatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono.

Mwaka 2020, Bi. Harris aliamua kuilenga mbalamwezi akiamini hata kama akiikosa atatua kwenye nyota, kwahiyo hatatoka ‘kapa’. Hayo ndiyo mahesabu ya wenye akili nyingi na maarifa. Aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuusaka urais wa Marekani, akaweka jina lake kati ya wanaowania nafasi ya kuwa wagombea kupitia Chama Cha Democratic.

Utayari wa Mapokezi ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris.

Lakini, kama unavyojua, wazee hawakosekani kwenye chama. Wakamuweka sawa, akaamua kuondoa jina lake. Joe Biden akamchagua kuwa mgombea mwenza, na wawili hao wakashinda uchaguzi wa urais wakimshinda Rais aliyekuwa madarakani, Donald Trump na Makamu wa Rais, Mike Pence.

Usiku wa leo, ataingia Tanzania kwa lengo la kudumisha uhusiano kati ya Marekani na nchi hii yenye utajiri mwingi wa asili na ndoto ya kuwa ‘nchi hisani’. Bi. Harris anatarajiwa kufika nchini saa nne usiku. Angekuja kwetu kijijini tungemchinjia jogoo na kuhakikisha anakula filigisi, kwakuwa ndiyo heshima ya mgeni. Ukarimu wa watanzania ni asili yetu. Mgeni huja akiwa amebeba kifurushi cha zawadi, nasi tunampa  kifurushi cha ukarimu. Kwetu mgeni haji mikono mitupu, na haondoki mikono mitupu.

Sasa Bi. Harris anakuja na kifurushi kilichobeba nini?

Usikose kufuatilia kwa karibu hapahapa, Dar24 Media kupata kila kinachojili.

Kagera Sugar waikamia mechi ya Yanga
Waziri Mabula atoa maagizo upimaji wa Ardhi, uvamizi maeneo