Felix Tshisekedi amebadili historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akiwa Rais wa kwanza anayetoka kwenye chama cha upinzani, lakini pia Rais wa kwanza anayeachiwa madaraka kwa kushinda uchaguzi.

Rais Mteule Tshisekedi ni mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa nguli wa upinzani na mwanzilishi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress- Kifaransa ‘Union pour la Démocratie et le Progrès Social’ (UDPS), Étienne Tshisekedi.

Étienne Tshisekedi anakumbukwa kwa namna alivyoweza kuwapasua kichwa kwa ushindani wa aina yake marais waliopita tangu miaka ya 1980 alipokuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa pili wa DRC (zamani Zaire), Mobutu Sese Seko.

Rais Mteule Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55, alianza kujiunga na harakazi za siasa mwanzoni mwa miaka ya 1980 baada ya baba yake, Étienne Tshisekedi kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa kumkosoa hadharani Mobutu Sese Seko.

Étienne Tshisekedi, baba yake Rais mteule wa DRC, Filex

Kabla ya mwaka 1980, baba yake Felix, Étienne Tshisekedi alikuwa mtu muhimu kwa Mobutu tangu mwaka 1965 na alifanikiwa kuchaguliwa kushika nyadhifa za juu. Alishiriki kumsaidia Mobutu kumpindua Rais wa wakati huo, Joseph Kasa-Vubu. Lakini kwa miaka ya 1990 alishiriki tena kampeni za kumuondoa madarakani Mobutu.

Étienne ana historia ya kushika nyadhifa za juu Serikalini huku akijitengenezea pia umaarufu mkubwa kwenye ulingo wa siasa dhidi ya Serikali. Aliwahi kushika nafasi ya Uwaziri Mkuu kwa vipindi vifupi katika mwaka 1991, mwaka 1992-1993 na mwaka 1997.

Mwanasiasa huyo nguli aliingia kwenye mgogogo mzito na Mobutu baada ya mwaka 1980 alipoanza kukosoa hadharani utawala wa kiongozi huyo anayetajwa kuwa dikteta.

Felix alilazimika kusitisha masomo yake na kuungana na baba yake katika kifungo hicho cha nyumbani kijijini kwao, katikati ya Kasai. Waliishi chini ya kifungo hicho hadi mwaka 1985 ambapo Mobutu alimuachia huru Tshisekedi na kumruhusu yeye na familia yake kuondoka Kasai.

Familia hiyo ilihamia Brussels nchini Ubelgiji ambapo waliishi kwa muda mrefu lakini hawakuacha kufanya siasa zilizoilenga DRC. Wakiwa nchini humo, Felix alianza kujikita katika masuala ya siasa na akawa mpiganaji wa kunadi sera za UDPS.

Mwaka 2008, Felix alianza kukabidhiwa mikoba ndani ya chama hicho, akichaguliwa kuwa Katibu wa Taifa wa Uhusiano wa Mambo ya Nje.

Novemba 2011, alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mbuji Mayi lililoko Kasai.

Hata hivyo, Felix alikataa kuingia bungeni akieleza kuwa hataki kukalia kiti cha ubunge unaotokana na uchaguzi uliochakachuliwa unaounda Serikali isiyo halali kidemokrasia.

Msimamo wa Felix uliendelea hata mwaka 2013 alipoteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI). Uteuzi wake ulitokana na sheria ya uchaguzi inayoruhusu wajumbe wa vyama vya upinzani kuwa sehemu ya Tume hiyo. Aliukataa uteuzi huo akisema, “sitaki kuweka kazi yangu ya siasa katikati ya mashuka.”

Kutokana na kujijengea jina kubwa na umaarufu wa kisiasa, mwaka 2016 UDPS walimchagua kuwa Makamu wa Rais wa chama hicho, huku baba yake akiendelea kuwa Mwenyekiti.

Hatua hiyo ilikuwa kama sehemu ya kumuandaa, kwani Machi 31, 2018 mwaka mmoja baada ya kifo cha baba yake, Felix alichaguliwa rasmi kuiongoza UDPS na kupewa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Hata hivyo, Novemba mwaka jana ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, vyama vya siasa vya upinzani vilianza mazungumzo ya kuungana kumsimamisha mgombea mmoja kwa lengo la kumshinda mteule wa Rais Joseph Kabila, Emmanuel Shadary.

Felix Tshisekedi alikuwa mgombea wa kwanza pamoja na Vital Kamerhe kusaini makubaliano ya kumuachia mfanyabiashara wa mafuta, Martin Fayulu kugombea wakimuunga mkono. Hata hivyo, Novemba 12 ilitangazwa kuwa makubaliano hayo yamefutwa.

Hivyo, Felix hakuwa anatazamwa zaidi kwa kulinganisha na Fayulu ambaye alionekana kuungwa mkono zaidi kwa upande wa upinzani; lakini upepo wa siasa ulibadilika na jahazi la Felix limefanikiwa kuvuka kwa haraka na uhakika hadi ng’ambo ilipo Ikulu ya DRC kupitia uchaguzi uliofanyika Desemba 30 mwaka jana.

Saa chache zilizopita, CENI ilimtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Desemba mwaka jana, akiwa na asilimia 38.5 ya kura zote na akijikusanyia takribani kura milioni 7 huku Fayulu akimfuatia kwa kura milioni 6.4 na mteule wa Rais Kabila, Emmanuel Shadary akiambulia kura Milioni 4.4.

Hatimaye, Felix Tshisekedi anasubiri kuapishwa kuwa Rais wa Tano wa DRC Januari 25 mwaka huu. Anapokea mikoba ya Urais kutoka kwa Joseph Kabila ambaye amekuwa Rais kwa miaka 18 tangu aliposhika madaraka baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa mwaka 2001.

Serikali: Marufuku shule binafsi kufukuza wanafunzi kisa ada
Ado awalipua Bashe na Nape 'Muswada unawahusu hawa'