Kaimu Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ruth Minja amesema kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kwa kipindi cha mwezi Julai 2019 kimebaki kuwa asilimia 3.7, kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2019.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa, kiwango hicho kubaki sawa kimechangiwa na kupungua kwa bei kwa baadhi ya vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kilichoisha Julai 2019.

Amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai 2019, umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 2.9 kutoka asilimia 2.3, ilivyokuwa kwa mwezi Juni 2019.

“Baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi Julai zikilinganishwa na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi (6.0%), unga wa mhogo (4.0%), mafuta ya kupikia (8.9%) na mbogamboga (4.6%) ambapo kwa upande wa bidhaa zisizokuwa za vyakula ni pamoja na vifaa vya kieletroniki, majiko ya gesi pamoja na vifaa pamoja na bidhaa za huduma,” amesema Minja

Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki, taarifa inaonyesha kuwa nchi ya Kenya ilikuwa na Kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kwa mwezi Julai 2019, ambapo kiwango chake kilifikia asilimia 6.27 ikilinganishwa na asilimia 5.70 kwa mwaka ulioishia Juni 2019.

Mchunguzi Mkuu Takukuru alivyodakwa kwa rushwa, utakatishaji fedha
RC Makonda aonya kuhusu Coco Beach, 'Hii hujuma haikubaliki'