Agustino Moshi (70), mfungwa mwenye namba 648/2015 aliyekuwa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa ubakaji, ameamua kujiua kwa kutumia wembe baada ya kujikata mshipa wa fahamu shingoni mara tatu akiwa ndani ya Gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo limetokea Jumatatu ya Juni 25 ndani ya gereza hilo na kushuhudiwa na mkuu wa gereza hilo, Kamishina Msaidizi wa Magereza (ACP), Leonard Moshy na kusema hajawahi kuona tukio hilo akisema ni la ajabu.

“Ni kweli alijikata mwenyewe akafa. Mimi sikuhadithiwa nililishuhudia mwenyewe. Sijawahi kuona mtu mwenye roho ngumu kama huyo. Yaani mtu anajikata damu zinatoka anajikata tu,” alisema ACP.

Ameongezea kuwa mzee huyo alitokea gereza la Maweni Tanga na kuletwa kwa rufaa kwa ajili ya kutibiwa KCMC sasa siku hiyo walizozana na ACP Moshy na ndio akaamua kujiua mbele yake.

Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, siku hiyo saa 8 mchana, mkuu wa gereza alifika ndani ya gereza kwa lengo la kuwapangia wafungwa kazi ya kwenda shambani, lakini mzee huyo akadai anaumwa.

“Huyo mzee alimwambia bwana jela (ACP Moshy) kuwa ana ED (kibali cha daktari cha kupumzika) lakini bwana jela akakataa na ndipo huyo mzee akasema basi ngoja afe tu,” alidokeza mtoa taarifa.

“Hapohapo akatoa kiwembe akaanza kujikata shingoni kwenye mshipa wa fahamu. Yaani anaushika anajikata damu zinatiririka. Kama mara tatu. Lilikuwa ni tukio la ghafla ambalo kila mtu hakulitarajia”.

Hata hivyo baadaye askari magereza walifanikiwa kumkimbiza katika zahanati ya gereza kwa ajili ya matibabu ya kuokoa maisha yake, lakini hata hivyo kutokana na majeraha hayo alifariki dunia.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Gabriel Chisseo alilithibitishia Mwananchi jana juu ya kupokelewa kwa mwili huo na kwamba hadi jana, bado ulikuwa umehifadhiwa hospitalini hapo.

“Yapo matukio yanayoweza kujitokeza gerezani sijawahi kuona tukio la aina hii wala hatujui kiwembe alikitoa wapi. Kuna mwingine aliwahi kujitumbukiza kwenye sufuria ya uji,” alisema.
Alipoulizwa iwapo kiini ni yeye kumlazimisha aende shamba, ACP Moshy alikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mfungwa huyo ni mmoja wa wafungwa ambao walikuwa hawataki kufanya kazi.

“Hawezi kulazimishwa. Mfungwa yeyote lazima afanye kazi. Hata mheshimiwa Rais (John Magufuli) amesema wafungwa wafanye kazi kwa hiyo ukija na kitambi utafanya kazi tu,” alieleza ACP Moshy.

Mfungwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa ubakaji mwaka 2015.i.

Rais Magufuli aenda Chato kwa mapumziko
Zitto: Tunafahamu Raphael alipo, Utekaji ni ushamba