Makumi ya vijana wamekimbia makazi yao baada ya baadhi yao kujeruhiwa na mgambo waliofika katika kijiji cha Yakobi mkoani Njombe, wakiwataka vijana hao kujiunga na mafunzo yao.

Baadhi ya vijana wa kijiji hicho wameeleza kuwa wamekumbana na kikundi cha mgambo hao bila kupewa taarifa, hali ambayo imesababisha fujo kati yao.

Imeelezwa kuwa kundi hilo la mgambo lilikuwa linatembelea maeneo ya starehe kama mabanda ya kuonesha mpira na vilabu vya pombe na kufunga milango, kisha kuwataka kijana mmoja mmoja kutoka nje na kujiunga nao.

“Nilipojaribu kutoka nje ya ukumbi, nikijaribu kusukuma mlango na wenzangu wakawa wamekuja kunisaidia, ile napata nafasi ya kutoka mlangoni nikapigwa na kitu chenye ncha kichwani na damu zilinivuja. Lakini baada ya kuangalia vizuri nikamuona Katibu Kata akiwa ameongozana na mgambo,” kijana aitwaye Mensod Luvanzila anakaririwa na Mtanzania.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Noel Mng’ong’o alisema kuwa idadi hiyo ya vijana walikimbia makwao wakihofia kuchukuliwa na mgambo hao, na kwamba ingawa nia ya mgambo hao ni nzuri kitendo cha kutowashirikisha vyema viongozi na kutoa taarifa ndicho chanzo cha tatizo.

“Kwa taarifa kamili, vijana 30 wamekimbia na sababu ni mgambo. Mgambo hawa kuja kwao ni kama ushirikishwaji haukuwepo ndani ya kijiji na viongozi,” anakaririwa mwenyekiti huyo wa kijiji.

Hata hivyo, Kaimu Afisa Tarafa wa Kata ya Imalinyi, Fadhili Mgaya ameelaani vitendo vya mgambo hao kutumia nguvu kupita kiasi katika zoezi lililohitaji hiari.

Alitoa wito kwa vijana ambao waliripotiwa kukimbia kijiji hicho kurejea ili waweza kuendelea kufanya kazi za kujenga Taifa.

NB: Picha iliyotumika siyo ya eneo la tukio,  ni kutoka maktaba

LIVE: Uzinduzi Tamasha la Urithi Festival
Atiwa mbaroni kutoa ofa vinywaji vyenye vilevi na kubaka wadada Dar, Mwanza, Arusha

Comments

comments