Aliyekuwa kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamis Mgeja ambaye alimfuata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alipotangaza kuhamia Chadema, amemfuata tena mwanasiasa huyo mkongwe akirejea CCM.

Mgeja ameweka wazi uamuzi wake leo alipozungumza na waandishi wa habari akiwa na familia yake, ambapo amedai kuwa haoni tena sababu ya kubaki Chadema.

Amesema kuwa uamuzi wake umetokana na kazi nzuri anayoifanya Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani, ambayo ilikuwa ndoto yake kuiona ikifanywa na kiongozi wa nchi.

Mgeja ametaja baadhi ya mambo mazuri ya Rais Magufuli yaliyomshawishi kuwa ni pamoja na kupambana vilivyo na ufisadi na rushwa; kurejesha nidhamu kwa nchi na chama.

Aidha, mwanasiasa huyo alirusha makombora kwa Chadema akidai kuwa ni chama kilichojaa ubinafsi na hakishauriki.

“Hawashauriki, mimi niliwashauri waendeshe chama kisiasa lakini wao wamebaki kuendesha chama kiharakati. Chadema wamejaa ubinafsi mkubwa uliotamalaki wa viongozi,” alisema Mgeja.

“Mfano nikiwa Ukawa, wanayo habari yao walienda kuwinda pamoja na vyama hivyo yaani NCCR-Mageuzi, NLD, CUF vilitumia nguvu kubwa kuunga mkono chadema na kuipa nguvu kubwa ya ruzuku huku vyama vingine hivi sasa haviambulii hata senti moja,” aliongeza.

Mgeja alikuwa miongoni mwa wafuasi wa CCM waliomfuata Lowassa alipotangaza kuhamia Chadema baada ya jina lake kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha walioomba kuwania urais kupitia chama hicho tawala mwaka 2015.

Alipewa nafasi ya kugombea urais kupitia Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa na alipigwa ‘debe’ kubwa na Mgeja.

Wiki iliyopita, Lowassa alitangaza kurejea CCM akitoa sababu kwa ufupi kuwa, “nimerudi nyumbani.”

Real Madrid yamnyapia Mbappe ikimtema Bale
Maelfu wakwama uwanja wa ndege Kenya, wafanyakazi wagoma