Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) umeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA) yaliyomalizika Disemba Mosi kwenye Viwanja vya Samora Mjini Iringa.

Katika mashindano hayo, Mgodi wa Dhahabu Geita umeibuka washindi wa Jumla kwenye mpira wa miguu Wanaume, Volleyball wanawake pamoja na Riadha wanaume mita 100 na Riadha wanaume Mita 200.

Aidha, GGM imeshika nafasi ya pili katika riadha kwa upande wa wanawake mita 200 na mchezo wa Basketball wanaume. Kampuni hiyo imekuwa mshindi wa Tatu kwenye Riadha wanawake mita 400 pamoja na Mita 800.

Akizungumzia ushindi huo, Meneja Mawasiliano na Mahusiano  wa Mgodi huo, Tenga B Tenga amesema kuwa ushindi huo ni uthibitisho kuwa Mgodi wa Dhahabu Geita unathamini michezo na kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Tano kuinua michezo Tanzania.

“Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania ni michezo muhimu inayoimarisha uhusiano baina ya wafanyakazi kutoka Taasisi mbalimbali, Kampuni yetu imekuwa ikishiriki kila mwaka kwenye michezo hii ili kujenga afya bora kwa wafanyakazi wake na kujenga ujirani mwema kati ya Kampuni hiyo na Mashirika ya Umma nchini,” amesema Tenga.

Hata hivyo, mashindano hayo yalizinduliwa rasmi tarehe 22 November mwaka huu na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na Kombe la ushindi lilikabidhiwa kwa timu ya GGM na Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza desemba 1 mwaka huu.

Video: Majeshi ya Umoja wa Afrika Mashariki kujifua kwa siku 17
Zanzibar Heroes yafanya kufuru Kenya