Mgogoro wa madaraka nchini Sudan Kusini umesababisha mabadiliko yanayoweka makamu wanne wa Rais, ili kuridhisha pande zinazosigana ambazo ni Serikali, waasi pamoja chama cha upinzani.

Uamuzi huo umetangazwa jana na Serikali ya nchi hiyo kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa maridhiano uliofanyika nchini Uganda ukiwakutanisha Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar.

Imeelezwa kuwa Riek Machar atakuwa makamu wa kwanza wa Rais akiongeza idadi kwa makamu wawili wa Rais waliopo hivi sasa, lakini pia ataongezeka makamu mwingine wa rais mwanamke kutoka chama cha upinzani.

“Tumekubaliana kuwa kutakuwa na makamu wanne wa rais; yaani wawili waliopo hivi sasa na ataongezeka Riek Machar ambaye atakuwa makamu wa kwanza wa rais, na pia nafasi ya nne atapewa mwanamke kutoka upande wa chama cha upinzani,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje, Al-Dierdiry Ahmed.

Kikao cha majadiliano kilichofanyika Kampala kililenga katika kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka minne nchini Sudan Kusini.

Al-Dierdiry Ahmed, alisema kuwa Rais Salva Kiir na kiongozi huyo wa waasi wamekubaliana kuhusu hilo na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baada ya kufanya makubaliano mengine yatakayofanyika jijini Khartoum na Nairobi nchini Kenya siku chache zijazo.

Mgororo wa madaraka nchini Sudan Kusini umesababisha vita vilivyochukua maisha ya makumi elfu na kuwalazimu mamilioni kuyakimbia makazi yao tangu Disemba 2013.

Neymar alia na kipigo cha Ubelgiji, ajiuliza kurejea PSG
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 9, 2018