Jeshi la polisi Mkoa wa Simiyu limesema kuwa mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi kupitia ACT – Wazalendo, Masunga Ng’ozo aliyepotea tangu Septemba 27 mwaka huu, alitekwa na watu wasiojulikana wanaomshikilia hadi sasa.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, Gemini Mushy alisema kuwa watekaji wamekuwa wakituma jumbe mbalimbali kupitia simu ya mgombea huyo kwenda kwa wazazi wake wakieleza kuwa wanahitaji kupewa kiasi cha shilingi milioni mbili na nusu ili kumuachia.

Kamanda Mushy alieleza kuwa watekaji hao wamekuwa wakitishia kuwa endapo pesa hiyo haitatumwa kwa muda wazazi hao wawe tayari kuupokea mwili wa mtoto wao kwa kuwa watamuua.

Akizungumzia mazingira ya kupotea kwa Bwana Mg’hozo, Kamanda Mushy alieleza kuwa alitoweka Septemba 27 majira ya mchana alipokuwa katika eneo la ofisi ya chama hicho. Alisema kuwa mgombea huyo alikuwa akiongea na simu akiwa amebeba begi lake huku akiwataka dereva wake pamoja na fundi mitambo kumsubiri huku akielekea sehemu fulani na hakurudi baada ya hapo.

Kamanda Mushy amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu hao na kumuokoa mgombea huyo wa ATC – Wazalendo.

Masunga Ng’hozo, ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), tawi la Mbeya.

 

 

Kituo Cha Kulea Na Kukuza Vipaji Kufunguliwa Dar
Mashabiki Wakiri Kuchoshwa Na Brendan Rodgers