Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya CCM, Philemon Mollel amepinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi wa kishindo, Godbless Lema wa Chadema.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya msimamizi wa uchaguzi huo kutangaza matokeo, Mollel alidai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa ambao unafanya matokeo hayo kutokuwa halali.

Alisema kuwa wakati zoezi la kupiga kura likiendelea kuna gari lililokamatwa likiwa na kura bandia za kumpa ushindi Lema ingawa alidai gari hilo liliachiwa baadae.

“Kulikuwa na Noah ya diwani wa Chadema ambayo ilipita katika baadhi ya vituo vya kupigia kura na kudai kupeleka vyakula. Lakini gari hiyo tumeambiwa ilikuwa na kura za bandia zilizofanikiwa kuingizwa kwenye masanduku,”alisema Mollel.

Kadhalika, alieleza kuwa kulikuwa na mapungufu makubwa kwenye fomu za matokeo kwa kuwa baadhi ya fomu hazikuonesha idadi ya kura zilizopigwa.

Mollel alilirushia lawama jeshi la polisi kwa madai kuwa liliwatisha akina mama na wazee kwenda kupiga kura.

“Hakukuwa na vurugu zozote, kwanini kuwatishia wanachi kwa silaha na vifaa vya kivita,” alihoji Mollel.

Matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili, Disemba 13 yalimpa ushindi Godlbess Lema kwa kupata kura 68,848 sawa na asilimia 65.9 huku Philemon Mollel akipata kura 35,607 sawa na asilimia 34 ya kura zote halali zilizohesabiwa.

Kubenea Afikishwa Mahakamani, Chadema watoa Tamko dhidi ya Uamuzi wa Makonda
Walioukataa uwaziri wa Magufuli Wafunguka sababu