Mwanasheria Alex Mgongolwa ameikingia kifua Kamati ya Uchaguzi ya TFF, baada ya kuwaengua baadhi ya wagombea wa nafasi ya Urais na Ujumbe wa Kamati ya Utendaji kwa kigezo cha kukosa wadhamini.

Kamati ya uchaguzi kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Benjamin Karume, ilitangaa kuwaengua wagombea 10, ambao walithibitika kukosa sifa za kuendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Mkoani Tanga mapema mwezi Agosti.

Mgongolwa amesema kanuni ya udhamini kwa wagombea kilichoibua sintofahamu, ipo kwa mantiki ya kisheria na ina lengo la kumpima mgombea anakubalika kwa kiasi gani, kabla ya kuendelea na mchakato wa Uchaguzi.

“Kila kanuni kwenye sheria ina mantiki, kuwa na wadhamini ni dhamira ya kupata uhalali na kuonyesha ni kiasi gani unaungwa mkono, binafsi naona ni sahihi,” amesema Mgongolwa.

Kuhusu elimu kwa wagombea, Mgongolwa ameunga mkono akisisitiza umuhimu wa elimu katika kuongoza shirikisho hilo akishauri wadau kutofanya jitihada kupingana na kipengele hicho.

Wagombea walioenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi za Urais kwa kutokidhi vigezo vya kikanuni ni Ally Mayay, Oscar Oscar na Ally Salehe.

Kwa upande wa nafasi ya Ujumbe walioenguliwa ni Liston Katabazi,  Jimmy ‘Kindoki’ Msindo, Saady Khimji, Thabit Kandoro, Denis Manumbu, Joseph Ngunangwa na Mrisho Ramadhan.

Dawa za kulevya kilo 88.27 zatelekezwa
Serikali yatoa kauli uchaguzi mkuu TFF