Osma Shariff, mtu wa kwanza kuthibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona (covid-19) nchini Kenya katika Kaunti ya Isiolo, amepanga kuiburuza Mahakamani Serikali ya Kaunti hiyo akiidai fidia ya Sh.25 milioni za Kenya.

Shariff mwenye umri wa miaka 62, amesema kuwa alipata matatizo makubwa ya kunyanyapaliwa na kupoteza wateja wengi katika biashara yake baada ya wafanyakazi wa idara ya afya kuweka picha yake kwenye mitandao ya kijamii.

Amewatuhumu wafanyakazi wa Hospitali ya Garbatula alipokuwa amelazwa katika eneo maalum (karantini) kuwa walimpiga picha na baadaye kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Hivyo, amepanga kufungua mashtaka akiitaka Serikali ya Kaunti hiyo kumlipa fidia kwakuwa wao ndio waajiri wa wafanyakazi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Mji wa Isiolo, Shariff alisema kuwa hivi sasa amepona kabisa, ameshapima mara mbili na ameonekana hana tena maambukizi ya covid-19.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa bado anaugua zaidi maradhi ya kisaikolojia kwani watu wengi wameona picha yake kwenye mitandao ya kijamii na humnyanyapaa.

Mzee Shariff ni mfanyabiashara anayemiliki duka kubwa la kuuza bidhaa za jumla na anamiliki pia mabasi kadhaa ya kusafirisha abiria kati ya Garbatula na Maua.

Amelalamika kuwa abiria wamekuwa wakibagua magari yake katika siku za soko na pia wateja wake wa kila siku wameacha kununua bidhaa kwenye duka lake wakihofia kuwa ana covid-19.

Ameongeza kuwa kuna wakati alisafiri na alipojaribu kutafuta nafasi ya kulala katika nyumba za kulala wageni aliambiwa sehemu zote kuwa vyumba vimeshachukuliwa hata kama vilikuwa wazi.

Zaidi, Shariff anasema kuwa hatua hiyo pia imeiathiri familia yake kwa sababu binti yake alinusurika kupigwa katika Mji wa Maua kwa madai kuwa kuwa anatoka kwenye familia yenye covid-19 na hakuwa amejikarantini.

Gavana wa Isiolo, Mohamed Kuti alilaani kitendo cha kuweka mtandaoni picha ya Shariff hususan jina lake kamili na namba ya kitambulisho chake.

Gavana Kuti alikiri kuwa mlalamikaji alipata madhara ya kisaikolojia na kwamba kwa niaba ya Serikali ya Kaunti hiyo, anamuomba radhi Shariff na familia yake.

Tanzania kufika Uchumi wa Juu, sekta ya madini yavunja rekodi ya miaka 4

Marufuku ya uuzaji wa pombe Afrika Kusini yarejea kukabili Corona

Bill Gates aeleza dawa ya corona inavyopaswa kusambazwa
Tanzania kufika Uchumi wa Juu, sekta ya madini yavunja rekodi ya miaka 4