Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba ametoa wito kwa wakulima Mkoani Simiyu kuondokana na dhana potofu kuwa matumizi ya mbolea yanazeesha ardhi badala yake wazingatie matumizi sahihi ya mbolea katika kilimo ili kuongeza mavuno, tija na uzalishaji katika kilimo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wilayani Itilima Mkoani Simiyu, katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Bukingwaminzi kata ya Zagayu wilayani humo wakati wa ziara yake ya kikazi.

Amesema kuwa siyo kweli kwamba matumizi ya mbolea yanazeesha ardhi badala yake mbolea inasaidia kutibu ardhi na kupelekea wakulima kuongeza mavuno na tija katika uzalishaji wa mazao na kuwawezesha kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Nimeambiwa hamtaki kutumia mbolea kwa madai kwamba mkitumia mbolea inazeesha ardhi siyo kweli, mbolea hizi haziharibu ardhi yetu bali zinakwenda kutibu ardhi ndiyo maana watu wa Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya , Songwe, Rukwa na Katavi wanaongoza kwa kuzalisha mahindi nchini, wenzetu ni wajanja wanatumia Mbolea,”amesema Mgumba

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amezungumzia suala la bei ya pamba ambapo amesema kuwa Serikali inaendelea kuandaa mazingira wezeshi kwa wanunuzi wa pamba wa ndani na nje ya nchi kununua pamba ya wakulima kwa bei nzuri na kubainisha kuwa utaratibu utakaotumika ni wa soko huria.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Silanga pamoja na kuomba pamba iuzwe kwa bei ya soko huria na kuongezewa viuatilifu, ameomba maghala ya kuhifadhia pamba yajengwe kupitia sehemu ya fedha inayotolewa na wakulima katika Vyama vyao vya Ushirika ili pamba ihifadhiwe vizuri na tija ionekane.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi amesema jitihada zinaendelea kufanyika kuwahamasha wakulima wote wa pamba kujiunga na vyama vya ushirika ambapo amesema hadi sasa ni wakulima 11,700  kati ya  38,910 wako katika vyama vya ushirika vipavyo 56.

Nao baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kuwasilisha maombi na kero zao kwa Naibu Waziri wa Kilimo wameomba viuatilifu/viuadudu vilivyotolewa na bodi ya pamba viwafikie wakulima  kwa wakati.

 

Video: Katoliki watoa waraka mzito, Hukumu ya kifo.
Breaking news: Ephraim Kibonde wa Clouds FM amefariki dunia