Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda ameweka wazi kuwa, mkakati wake kwa sasa ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo kwa lengo la kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.

Mgunda ametoa kauli hiyo wakati Young Africans ikiongoza Msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 35 sawa na Azam FC lakani wanatofautiana mabao ya Kufunga na Kufungwa, huku Simba SC ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 34.

Kocha Mgunda amesema anachotaka kwa sasa ni kukiona kikosi chake kikipambana maradufu ili kupata alama tatu za kila mchezo, kwa kuamini ndio njia sahihi kwa klabu hiyo ya Msimbazi kufikia lengo la Kutwaa Ubingwa.

Amesema kinyume na hapo mambo yatakua magumu sana kwake na kwa Simba SC, ambayo msimu uliopita ilipoteza Taji la Ligi Kuu mikononi mwa Watani zake wa Jadi Young Africans.

“Kikubwa tunachokitaka kwa sasa ni kuweka nguvu zaidi kwenye michezo yetu kwa kuhakikisha kila mchezo tunashinda, kwa sababu Ligi imekua na ushindani mkubwa na tukizubaa hali itakua mbaya kwetu na ubingwa tutaukosa.”

“Unajua Ligi Kuu msimu huu imekua tofauti sana na misimu iliyopita, ndio maana unaona kila timu inajituma kwa kucheza kwa kujihami na kushambulia, hii yote ni kutotaka kuangusha alama ama kupata sare hasa suala la ushindi linapohitajika kwa timu shiriki.”

“Kwa hiyo kwa kikosi changu cha Simba SC tunatakiwa kujiandaa kwa hali yoyote ile ili tufanikishe lengo la kuapata alama tatu za kila mchezo kutoka kwa wapinzani wetu.”

Ajali ya Cruiser gari la Jeshi na pikipiki: Vilio vyatawala msibani
Wasanii wahamasishaji matumizi Dawa za kulevya waonywa