Makali ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 yameendelea kuwakata wanaotuhumiwa kuivunja ambapo wiki hii mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (Muce), Dkt. Oscar Magavi amekuwa miongoni mwa watu kumi waliokamatwa tangu ianze kutumika..

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi aliwaambia waandishi wa habari kuwa jeshi hilo lilimtia mbaroni Dkt. Magavi akiwa Sumbawanga na baadae kumrudisha mkoani humo, baada ya kubainika kuwa alitenda kosa hilo Septemba 15 mwaka huu akiwa Iringa.

Hata hivyo, Kamanda Mjengi hakuweka wazi maneno aliyoyatumia mhadhiri huyo wa chuo kikuu yanayodaiwa kumkashifu Rais Magufuli akieleza kuwa bado wanaendelea na upelelezi.

Dk. Magavi amekuwa mtuhumiwa wa 10 kukamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za makosa ya kimtandaoni ambapo watuhumiwa wengine wanaendelea na kesi mahakamani.

Mapema mwezi Juni, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi milioni saba Isaac Emily baada ya kumkuta na hatia ya kumtusi Rais John Magufuli mtandaoni. Kijana huyo alilipa faini hiyo na kuahidi kutorudia kosa hilo.

Video: DC Mjema - Serikali ipo macho, Atoa mikakati kupambana na uhalifu Ilala
Mambo 10 ya kufanya kabla hujafikia miaka 28