Mhadhiri wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo amepandishwa kwenye kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Agosti 14, 2019 na kusomewa mashtaka ya kudai rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa chuo hicho.

Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vera Ndeoya ameiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Januari 12, 2017 katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Com David iliyoko Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ndeoya ameeleza kuwa mtuhumiwa alifanya kosa hilo akiwa mwajiriwa wa NIT kama mhadhiri aliyekuwa akifundisha masomo ambayo msichana huyo alikuwa anasoma. Alieleza kuwa mhadhiri huyo aliomba rushwa ya ngono akiahidi kumsaidia msichana huyo kufaulu masomo.

Alieleza kuwa mtuhumiwa alitumia madaraka yake vibaya kuomba rushwa ya ngono akijua ni kinyume cha sheria na maadili ya kazi yake.

Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo. Aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 17, 2019. Mwanasheria wa Takukuru aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Tuhuma hizi dhidi ya mhadhiri wa NIT, ziliwahi kuripotiwa pia kwa mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dodoma, Jacob Nyangusi ambaye alikamatwa Oktoba 4, 2018 akidaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza akiahidi kumsaidia katika masomo.

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.

Mke wa bondia Cheka afunguka taarifa kuhusu mumewe na ajali ya moto Morogoro
Mwili wa marehemu wafukuliwa nchini Kenya