Katika kuelekea Maadhimisho ya Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika Aprili 26, 2017 katika Viwanja vya Jamhuri Mjini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema kuwa maandalizi hayo yamekamilika.

Ameyasema hayo mapema hii leo wakati akizungumza waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Mjini Dodoma.

“Nipende kuwaeleza Watanzania wote kuwa hadi sasa maandalizi ya kufikia siku ya Maadhimisho ya Sherehe za Muungano tayari yamekamilika kwa kuangalia mambo yote yaliyopangwa katika ratiba ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli.”Amesema Mhagama.

Aidha, amesema kuwa sherehe hizo zitakuwa za kipekee na za aina yake ukizingatia kuwa  zinafanyika kwa mara ya kwanza tangu Serikali ilipotimiza adhma yake ya kuhamia Dodoma.

Mhagama ameongeza kuwa sherehe hizo zitapambwa na Gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, maonyesho ya Kikosi cha Makomando, Onyesho la Mbwa na Farasi waliofunzwa, onyesho la ukakamavu la Uzalendo la Wanafunzi kutoka shule za Sekondari za Dodoma.

Kwa upande wake,   Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba  ametoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza  kwa wingi kwenda  kuangalia mafanikio yaliyotokana na uwepo wa Muungano huo.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Jordan Rugimbana amepongeza jitihada za Ofisi ya Waziri Mkuu hususani Kitengo cha Maadhimisho kwa kushirikiana na Ofisi yake kuratibu na kuhakikisha maandalizi yote yamekamilika kwa wakati uliopangwa.

 

Uongozi Simba wateta na Waziri Mwakyembe
Video: Majina watakao wania tuzo EJAT yatangazwa